Na. Majid Abdulkarim, Dodoma
Wananchi wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya dawa kwa kutonunua dawa bila kuwa na cheti cha Daktari pamoja na maeneo yasiyo sajiliwa ili kuweza kupunguza usugu wa dawa unaosababishwa na matumizi holela ya dawa.
Wito huo umetolewa leo jijini Dodoma na Msajili wa Baraza la Famasi nchini, Bi. Elizabeth Shekalaghe ambaye pia ni Mlezi wa Chama cha Wanafunzi wa Famasi Tanzania katika mkutano wa 14 wa Mwaka wa chama hicho ikiwa pia ni kuelekea kilele cha Wiki ya Famasi.
Bi.Elizabeth amesema kuwa ni vema kwa wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya dawa ili kuhakikisha wanakuwa salama juu ya usugu wa dawa mwilini.
Bi.Elizabeth amesema kuwa katika kuelekea kilele cha wiki ya famasi anawakumbusha wafamasia wote nchini kuendelea kuzingatia maadili na miiko ya taaluma zao ili kuwasaidia wananchi na taifa kwa ujumla kuwa salama.
Akizungumza Bi. Elizabeth amesema Wafamasia wanaendelea kutekeleza majukumu yao katika kuangalia namna gani ya kuboresha huduma za kitabibu za kifamasia katika hospitali zote nchini
“Tunahitaji kufanya kazi tukiwa na weledi mkubwa ili wananchi waendelee kutuamini pamoja na uchache wetu nchini”, ameeleza Bi.Elizabeth
Ameeleza kuwa wafamasia nchini wako 3372 ambapo idadi hiyo bado ni ndogo katika kuwahudumia watanzania hivyo wanakazi kubwa na mchango mkubwa wa kuendelea kutoa katika sekta ya afya ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Naye rais wa Chama cha Wanafunzi wa Famasia TanzaniaNoel Shimba ameeleza kuwa kongamano hilo husaidia wanafunzi wanao soma ufamasia kupata ujuzi kutoka kwa wakubwa wao waliotangulia
Vile vile amesema kuwa husaidia kubadilishana mawazo na wanafunzi wenzao kutoka vyuo vingine nchini kwa lengo la kuborehs huduma ya ufamasia pale watakapo kuwa wanatumikia
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Chama cha Wafamasia Tanzania Prof. Eliagiringa Kaale amewataka wanafunzi wa chama cha ufamasia Tanzania kuwa na juhudi binafsi ili kuhakikisha wanalisaidia taifa katika kulinda afya zao.
No comments:
Post a Comment