Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde akitoa maelekezo mara baada ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya elimu katika shule ya sekondari Mwanzi iliyopo wilayani manyoni. |
Na: James Mwanamyoto – OR-TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Charles Msonde amewataka walimu wa elimu ya awali kuhakikisha wanawapatia watoto malezi bora na ujuzi ili wakianza darasa la kwanza wawe na msingi mzuri wa elimu.
Dkt. Msonde ametoa wito huo kwa walimu wote shule za awali nchini, wakati akifungua mafunzo ya walimu 105, Maafisa Elimu Kata 21 na Walimu Wakuu 21 wa Mkoa wa Singida ambayo yatakayowawezesha kutoa elimu yenye tija kwa watoto.
Dkt. Msonde amesema, Serikali inathamini elimu ya awali na ndio maana kupitia mradi wa BOOST madarasa ya awali 12,000 yatajengwa ili kuwezesha shule zote za msingi nchini kuwa na madarasa ya awali kwani miongoni mwa shule zote takribani 17,000 zilizopo baadhi yake tayari zina madarasa ya awali.
“Elimu ya awali inajenga msingi bora wa malezi ya mtoto, tabia nzuri, pamoja na utamaduni wa mtoto kupenda shule, na ndio maana Mhe. Rais aliridhia mradi wa BOOST utengewe trilioni 1.15 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu katika kipindi cha miaka 5 cha utekelezaji wa mradi huo,” Dkt. Msonde amefafanua.
Ameongeza kuwa, mradi huo umetoa fursa kwa walimu hao kujengewa uwezo wa kutoa mafunzo kwa watoto kwa kulingana na hatua za makuzi.
Kwa upande wake, kiongozi wa wawezeshaji, Dkt. Fortunata Pembe amesema, pindi walimu hao wakihitimu mafunzo hayo watakuwa tayari kutoa mafunzo kwa walimu wengine.
Naye, Mwalimu Kitila Mkumbo ambaye ni miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo, ameshukuru kwa kupatiwa mafunzo na kuahidi kuyatumia vizuri ili watoto wapate malezi bora na ujuzi.
No comments:
Post a Comment