ZAIDI YA BILIONI 8 ZATUMIKA KUBORESHA MTANDAO WA BARABARA WILAYANI ARUMERU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, March 13, 2026

ZAIDI YA BILIONI 8 ZATUMIKA KUBORESHA MTANDAO WA BARABARA WILAYANI ARUMERU



Na Mwandishi Wetu - Arumeru


Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) imeendelea kuboresha na kukamilisha ujenzi wa barabara mbalimbali katika Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha, hatua inayolenga kurahisisha usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.

Hayo yameelezwa na Meneja wa TARURA Wilaya ya Arumeru, Mhandisi Julius Kaaya, katika mahojiano maalum na waandishi wa habari.

Mhandisi Kaaya amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 8 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo.

Amefafanua kuwa wilaya ya Arumeru ina mtandao wa barabara zenye urefu wa takribani kilometa 1,550 zinazohudumiwa na TARURA, ambapo kilometa 797 zipo katika Halmashauri ya wilaya ya Arusha na kilometa 753 katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru.

Amesema kuwa fedha hizo zimetumika kujenga barabara za lami na zege (Mita 280) pamoja na madaraja matatu, ikiwemo madaraja mawili katika Halmashauri ya Arusha na daraja moja katika Halmashauri ya Meru.

Amesema kuwa kwa muda mrefu ujenzi wa barabara za lami katika wilaya hiyo ulikuwa ukikamilika kwa kiwango kidogo, ambapo Halmashauri ya Arusha ilikuwa na kilometa 14.1 na Halmashauri ya Meru kilometa 8.1. Hata hivyo, katika mwaka wa fedha 2024/2025 kumeshuhudiwa ongezeko la takribani kilometa 10 za barabara za lami kwa pamoja katika halmashauri hizo mbili.

Aidha, Mhandisi Kaaya amebainisha kuwa TARURA imekuwa ikijenga madaraja ya mawe ambayo yanasaidia kupunguza gharama za ujenzi kwa kiasi kikubwa, huku yakitoa ajira kwa wananchi wa maeneo husika kwa kuwa ujenzi wake hutumia mawe na rasilimali nyingine zinazopatikana katika eneo la mradi husika.

Ameongeza kuwa miundombinu ya barabara itasaidia pia shughuli za kiuchumi, hususan usafirishaji wa mazao ya kilimo kutoka mashambani kwenda sokoni, kwa kuwa wilaya ya Arumeru ni mzalishaji mkubwa wa mazao mbalimbali yanayosafirishwa kwenda mjini

Amesema barabara hizo zina umuhimu wa kimkakati kwa kuwa zinaunganisha mtandao wa barabara za Afrika Mashariki na hivyo kurahisisha mawasiliano na usafiri kati ya nchi za ukanda huo.

Kuhusu ushiriki wa vijana na wanawake katika miradi hiyo, Mhandisi Kaaya amesema TARURA imeweka utaratibu wa kuwajengea uwezo kupitia mafunzo kwa vikundi vilivyosajiliwa ili waweze kushiriki katika kazi ndogondogo za ujenzi wa barabara na hivyo kujipatia kipato.

Hata hivyo amewataka wananchi kutambua juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha miundombinu ya barabara na kuwataka kuilinda ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuwanufaisha wananchi wa sasa na vizazi vijavyo katika maendeleo endelevu ya wilaya ya Arumeru na Taifa kwa ujumla.

Naye, Bw. Jeremia Isanzya mkazi wa Machumba amesema awali walikua wakipata changamoto kwenye barabara hiyo ambayo ipo mlimani na pia iikua na korongo na hivyo kusababisha ajali wa wakazi hao.

“Tunashukuru serikali kwa kufanya kazi nzuri kwani sasa hivi watu na magari yanapanda na kushua,pia imesaidia watu kufika hospitali na kufika juu kupata huduma za mahakama na hoteli.



No comments:

Post a Comment