Na. Veronica Mwafisi-Bagamoyo
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewapongeza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kwa kusimamia na kuwahudumia vizuri walengwa wa Mradi wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao kwa asilimia kubwa umeinua maisha ya wananchi wa eneo hilo.
Mhe. Kikwete ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi na walengwa wa TASAF wa Kata ya Dunda, Kijiji cha Dunda katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.
“Kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora niwapongeze ninyi viongozi wa Halmashauri ya Bagamoyo kwa kujitoa kwenu katika kuwasimamia na kuwahudumia wananchi wa eneo hili la Bagamoyo,” Mhe. Kikwete amesema.
Mhe. Kikwete amesema kuwa, endapo halmashauri zote nchini Tanzania zitasimamia na kuratibu mradi wa TASAF kwa usahihi kama ambavyo halmashauri ya Bagamoyo inafanya, ifikapo mwaka 2026 nchi ya Tanzania itakuwa imeondokana na tatizo la wananchi kuwa na hali duni za maisha.
Aidha, Mhe. Kikwete amewataka wananchi na walengwa wa halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kumuombea Rais Mhe. Dkt. Samia Hassan kwa kuwa anafanya kazi kubwa ya kuhakikisha kila mwananchi anainuka kutoka katika hali duni na kuwa na maisha bora.
Kwa upande wake, mlengwa wa TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bi. Mwanahawa Sobbo ameishukuru TASAF kwa kumuinua kimaisha na kumuunganisha na vikundi ambavyo vimemsaidia kupata mkopo wa Halmashauri ya Wilaya ambao umewawezesha kununua machine ya boti inayofanya biashara na kuwaingizia kipato kikubwa.
Naye, Mlengwa mwingine wa TASAF, Bi. Mwanaheri Maulidi ametoa shukrani kwa Serikali kupitia mradi wa TASAF kwa kuinua maisha yake kwani ruzuku ambayo alikuwa akiipokea ilimuwezesha kusomesha watoto wake pamoja na kupata ada yake ya kwenda kujifunza ufundi cherehani.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amehitimisha ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Pwani iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao pamoja na kukagua utekelezaji wa Miradi ya TASAF.
No comments:
Post a Comment