Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Nandera Mhando, kwenye Picha ya pamoja na viongozi mbalimbali walioshiriki Uzinduzi wa Mradi wa HAPANA MAREFU YASIYO NA MWISHO jijini Dodoma Julai 03,2023 |
Na WMJJWM, Dodoma
Kamishna wa Ustawi wa Jamii Nchi Dkt. Nandera Mhando amesema Takwimu za utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria kupitia viashiria vya mwaka 2022 zinabainisha kwamba jumla ya wasichana 418 hawakumaliza elimu ya msingi kwa sababu ya mimba.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Ustawi wa Jamii nchini Dkt. Nandera Mhando, alipomwakilisha Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima Julai 03, 2023 jijini Dodoma kwenye Uzinduzi wa Mradi wa HAPANA MAREFU YASIYO NA MWISHO.
Dkt. Nandera amesema kwa mujibu wa taarifa ya Utafiti huo mwaka 2015/16 asilimia 27 ya wasichana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 19 wamepata ujauzito kwa mikoa ya katavi (45%), Tabora (43%), Dodoma (39%), Morogoro (39%) na Mara (37%).
Dkt. Nandera amesema kuzinduliwa kwa Mradi huo, chini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania kutaongeza wigo wa afua za kupambana na Ndoa za Utotoni hivyo ametoa rai kwa Viongozi wa Dini wakati mchakato wa kuzifanyia mabadiliko sheria mbalimbali ikiwemo sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ukiendelea, kutoe maoni yao ili yajumuishwe kabla ya kupelekwa Bungeni.
"Mimba za utotoni bado ni tatizo kubwa na kikwazo kikubwa kwa wasichana kukamilisha mzunguko wao wa elimu hapa nchini na ndoto zao. Mimba za utotoni licha ya kuzorotesha masomo ya mtoto wa kike, pia zina madhara ya kiafya yaani husababibisha ongezeko la vifo vya mama na mtoto hapa nchini. Amesema Dkt. Mhando na kuongeza
Akitoa Salaam za Kanisa, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, (KKKT) Dkt. Fedrick Shoo amesema, uzinduzi huo ni ishara kuwa Tanzania ina baraka za kipekee, kwani linapokuwa jambo linayoigusa Jamii wanafanya kwa pamoja.
"Sisi ni Tanzania kwanza, kama kuna jambo linamhusu mtoto wa kitanzania ni la kwetu sote bila kujali tofauti ya Dini zetu" amesema Dkt. Shoo.
Ameongeza pamoja na kazi yao kuu ya kueneza Injili, lakini pia wamekuwa wakitoa huduma za kijamii, kwa sababu hata Yesu Kristo Mwenyewe alizifanya, kwani sio sawa kuitwa Kanisa kama hatuwezi kumuhudumia Mwanadamu Kiroho Kimwili na kiakili " alisisitiza Dkt. Shoo.
Dkt. Shoo amesema, wanatamani kutokomeza Ndoa za Utotoni, na kuleta Mabadiliko ya kisheria.
"Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, tunaona inahitaji mabadiliko, mtoto wa kike wa Miaka 14, 16 au 17 hawa bado niwa Mtoto, hivyo tutashirikiana na Serikali kuona Mabadiliko yanatokea" ameongeza Dkt. Shoo.
Akitoa Ushuda wakati wa Uzinduzi huo wa Mradi Marefu Yasiyokuwa na Mwisho, Binti Elizabeth Sagath amesema, wapo wasichana wengi wanaotamani kufikia Ndoto zao lakini mila na Desturi zimekuwa kikwazo kwao.
"Mimi kwa sasa nasoma Chuo cha Diplomasia shahada yangu ya kwanza, lakini Baba yangu hakuwa tayari kuona ndoto zangu zinatimia kwani nilipo hitimu darasa la saba tu, alichukua Mahari ili mimi niolewe, walionisadia ni kanisa" alisema Elizabeth, aliyenusurika mara mbili kuozwa.
Akizungumzia Utekelezaji wa Mradi huo Mratibu wa Mradi, Patricia Mwaikenda amesema unategemea kuwafikia watoto wa kike 2400 kwenye Vijiji 24 na maeneo lengwa ni Zanzibar, Tabora, Morogoro, Mwanza na Dodoma.
Mradi wa Marefu Yasiyo na Mwisho utadumu kwa Miaka mitatu na utatumia Bil. 2.5.
No comments:
Post a Comment