Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya RITA, Dkt. Amina Msengwa aliwashukuru wadau mbalimbali wa maendeleo waliojitokeza na kutoa mchango wao katika kufanikisha mpango huu. |
Naibu Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu akitoa salamu za Wizara kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Bi Mary Makondo katika Hafla hiyo. |
Na Lusajo Mwakabuku – WKS KAGERA
Tangu kuzinduliwa kwa mpango wa usajili wa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ukiwa ni mkakati muhimu ulioanzishwa na Serikali chini ya uratibu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa lengo la kuboresha hali ya usajili wa vizazi nchini mwezi Juni, 2015 mpaka sasa, watoto zaidi ya 8,292,343 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.
Hayo yameelezwa leo tarehe 04/07/2023 na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul akisoma hotuba iliyoandaliwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ambaye ndiye aliyetakiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo na akawakilishwa na naibu wake kutokana na muingiliano wa majukumu mengine ya kiserikali katika uzinduzi wa mpango huo uliofanyika mjini Bukoba mkoani Kagera.
Akisoma hotuba hiyo, Mhe. Gekul alisema mpango huu ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu usajili wa watoto na akasisitiza kuwa ni lazima RITA wahakikishe mpango huu unafanikiwa hapa Kagera ili kufikia lengo la kitaifa la kila mtoto awe amesajiliwa ifikapo mwaka 2025.
“RITA mnatakiwa kusimamia na kuratibu utekelezaji wa mpango huu katika maeneo yote ya mkoa huu ili watoto wote wenye sifa wasajiliwe na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa. Mbinu mbalimbali zitumike ili kuhakikisha kwamba kila mtoto amepata huduma na ikiwezekana kupita nyumba kwa nyumba kufanya uhakiki” Alisema Gekul.
Pia Mhe. Gekul aliwaagiza RITA kutoa elimu na hamasa ya kutosha kwa wananchi kuhusu mpango huu ili wajitokeze kwa wingi kuwasajili watoto wao. Pia aliwataka kuwaelimishe wananchi juu ya uhalali wa vyeti hivi kwa matumizi yoyote na vinatolewa kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano lakini vitaendelea kutumika hata mtoto atakapovuka umri huo yaani ni cheti cha kudumu.
Maelekezo ya Waziri pia yalijikita kwa watendaji wa kata pamoja na watoa huduma wa vituo vya afya akiwataka wahakikishe wanafanya kazi kwa weledi, uadilifu na uzalendo wa hali ya juu huku wakiweka mbele maslahi ya Taifa na kutenda haki kwa wananchi wote huku akihimiza utunzaji na matumizi sahihi ya vitendea kazi vilivyotolewa hasa simu kwa kazi iliyodhamiriwa.
“Mwaka jana nikiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Mpango huu Mkoani Ruvuma yapo maeneo wasajili walinieleza kwamba simu ni mbovu lakini walipoileta tulibaini na kukuta anaitumia kwa mawasiliano binafsi. Nasisitiza vifaa hivi ni mali ya serikali hivyo ni lazima vitunzwe kama mali nyingine” aliongezea Naibu Waziri.
Akitoa salamu za Wizara kwa niaba ya Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Khatibu Kazungu alisema Kagera ni moja ya mikoa ya mwisho kuanza kutekeleza Mpango huu na kwamba jumla ya Watoto 418,246 wanatakiwa kusajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.
Akawataka watumishi wanaosimamiwa na RITA kuitumia faida ya kuwa wa mwisho kwani wameshajifunza mengi katika mikoa iliyotangulia na watumie uzoefu huo kurekebisha makosa yaliyofanyika katika mikoa mingine.
Akitoa salamu za shkrani, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya RITA, Dk Amina Msengwa aliwashukuru wadau mbalimbali wa maendeleo waliojitokeza na kutoa mchango wao katika kufanikisha mpango huu wakiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto - UNICEF, Serikali ya Canada na Kampuni ya Mawasiliano ya TIGO pamoja na wadau wengine kwa kuendelea kuwa sehemu ya utekelezaji wa mpango huu muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.
No comments:
Post a Comment