Na Shua Ndereka
Serikali katika malengo yake ya maonesho ya wakulima ‘nanenane’ kitaifa mwaka 2024 inatarajia kuzialika nchi za jirani kuja hapa nchini kuonesha bidhaa zao ili kubadilishana uzoefu na kujifunza mambo mbalimbali.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi David Silinde Agosti 02, mwaka huu, baada ya kutembelea mabanda mbalimbali katika maonesho ya wakulima maarufu kama nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere Manispaa ya Morogoro.
“Kama kutakuwa na jambo moja halijafanyika vizuri mwakani tutafanya vizuri zaidi, tutakuja na ubunifu kutokana na kazi nzuri hii tuliyoanza, malengo ya serikali kwamba mwakani tunataka kitaifa tualike nchi jirani mfano Kenya, Uganda, Rwanda waje nao waoneshe kile wanachokifanya hivyo wanunuzi, wasindikaji na wazalishaji wajifunze ” Alisema.
Katika hatua nyingine Silinde amewapongeza Viongozi na waandaji wa maonesho ya 30 ya nanenane Kanda ya Mashariki kuwa ni mazuri na yamelenga kusudio la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kufikisha ujumbe kwa wananchi.
Ametoa rai kwa wananchi katika kanda hiyo kuhudhuria na kutembelea maonesho hayo ili kuona yale yanayofanyika katika ngazi za halmashauri, Taasisi, Mikoa ili kuendeleza Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Awali akitoa maelekezo juu ya uvuvi haramu mara baada ya Naibu waziri Silinde kutembelea banda la Wizara ya Mifugo na uvuvi, Afisa Uvuvi Mwandamizi Grace Kakama, amewashauri wavuvi nchini kutotumia zana haramu katika shughuli zao za uvuvi ili kutunza mazingira na viumbe waishio baharini.
Amesema kuwa, zipo aina mbalimbali za uvuvi haramu ambazo ni matumizi ya nyavu zenye macho madogo, Matumizi ya Sumu, Kupiga Katuli, Matumizi ya nyavu za timba, vilipuzi ikiwemo mabomu yaliyotengenezwa kwa baruti na kokoro.
“Zana haramu tumezileta hapa katika maonesho haya ya nanenane ili kuwaelimisha wananchi kwamba wanapofikiria kwenda kufanya uvuvi ama kuwekeza katika sekta ya uvuvi basi watumie zana zilizoruhusiwa kisheria kwani zana hizo haramu huharibu mazingira ya baharini, samaki na hupunguza kiasi cha samaki kwa kiasi kikubwa” Alisema.
Naye Afisa Mifugo wa shamba la serikali (LMU) Boniphace Kipaya kutoka Shamba la kuzalisha mifugo la Ngerengere katika halmashauri ya wilaya ya Morogoro alisema kuwa changamoto za ufugaji wa ng’ombe hutokana na vile unavyofuga mifugo yako huku amewaasa wafugaji kuzingatia kanuni za ufugaji bora.
Naibu waziri David Silinde ametembelea mabanda mbalimbali na kushuhudia kazi zinazotekelezwa likiwemo banda la Bodi ya Pamba, Jeshi la Magereza, Halmashauri ya mji wa Ifakara, Halmashauri ya wilaya ya Gairo, Wilaya ya Lushoto, Muheza, Chalinze na Kisarawe.
No comments:
Post a Comment