PINDA: MUNGU ATATULAANI TUSIPOWATUMIKIA WANANCHI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, August 3, 2023

PINDA: MUNGU ATATULAANI TUSIPOWATUMIKIA WANANCHI


Na Shua Ndereka


Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Kayanza Peter Pinda amewataka wakuu wa Mikoa, wakuu wa wilaya na viongozi wengine kuwatumikia wananchi kwa moyo na kuzingatia maadili ya kazi.


Mizengo Pinda amesema hayo, Agosti mosi mwaka huu katika ufunguzi rasmi maonesho ya wakulima maarufu kama nanenane kanda ya Mashariki inayoundwa na mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Tanga na Pwani.


Akitoa hotuba yake ya ufunguzi mara baada ya kutembelea mabanda ya bidhaa mbalimbali katika maonesho kwenye Uwanja vya Mwalimu Julius Nyerere uliopo Nanenane Manispaa ya Morogoro, Waziri mkuu mstaafu Pinda amesema kuwatumikia watanzania ni lazima kiongozi kujikana kwa kutoa nafasi kubwa kwao.


Amewasisitiza viongozi waliokabidhiwa mikoa, wilaya na halmashauri kuweka maslahi ya wananchi nafasi ya kwanza, kutumia muda mwingi kuzungumza na kuwaelekeza nini kifanyike ili kuleta maendeleo.


“Viongozi wanapokuwa hawana maadili si waadilifu wamekabidhiwa dhamana lakini hawana uadilifu wowote, kwa hiyo baadhi ya mambo ambayo mnayaona hayasimamiwi vizuri, hivyo mkitaka kusimamia vizuri kazi ya kuwatumikia watanzania ni lazima wewe ujikane kwa kutoa nafasi kubwa kwao, na uhakikishe fedha zinazoletwa zinasimamiwa vizuri ili kuhakikisha lile lengo linatimizwa tusipofanya hivyo Mwenyezi Mungu atatulaani maana mimi sioni namna nyingine…”. Alisema Pinda



Aidha amewakumbusha jamii juu ya utunzaji wa Mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi, kutunza vyanzo vya maji na kusisitiza suala la upandaji wa miti kwa wingi.


Sambamba na hayo Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge na Mwenyekiti wa kamati katika maandalizi ya Maonesho hayo, alisema kuwa idadi ya washiriki wa maonesho ya mwaka huu imepanda tofauti na mwaka jana jambo linaloonesha mwakani kuwa na taswira tofauti.


Kunenge amesema mwaka huu wanategemea washiriki wa maonesho hayo kufikia 75 elfu ikilinganishwa na mwaka jana ambapo washiriki walikuwa elfu hamsini.


Awali akiwakaribisha wageni na kutoa salaam za mkoa wa Morogoro, Mkuu wa Mkuu Mkoa Adamu Malima alibainisha Malengo ya mkoa katika kilimo ni kuwa mkoa wa kimkakati katika mazao mbalimbali ikiwemo sukari, kahawa na Mpunga.



Malima ameongeza kuwa takwimu za mwaka jana katika uzalishaji wa mpunga Mkoa wa Morogoro ulizalisha mpunga tani laki tisa ambapo matarajio ya msimu ujao ni kuzalisha zaidi.


Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba ameeleza maana ya maonesho hayo ya nanenane kwamba ni fursa kwa wakulima, wafugaji na wavuvi katika kuonesha bidhaa zao, kutanua masoko pamoja na kupata mafunzo bora ya uendeshaji na kuzalisha kwa tija.


Hata hivyo Maonesho ya Nanenane kwa mwaka huu 2023 kitaifa yanafanyika jijini Mbeya huku yakibebwa na Kauli Mbiu isemayo Vijana na Wanawake ni msingi imara ya mifumo endelevu ya Chakula.

No comments:

Post a Comment