Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekanya ameupongeza Wakala wa Barabara nchini TANROADS mkoa wa Kigoma kwa kumsimamia vizuri mkandarasi STECOL Cooperation Ltd, anaejenga barabara ya Malagarasi-Ilunde- Uvinza km 51.1 kwa kuikamilisha kwa viwango.
Kukamilika kwa barabara hiyo sasa kunaifanya barabara yote ya Tabora-Kigoma km 413 kukamilika kwa lami.
Akizungumza wakati akikagua barabara hiyo Eng. Kasekenya amemtaka mkandarasi STECOL anaejenga barabara hiyo kukamilisha daraja la Ruchugi katika kipindi cha mwezi mmoja toka sasa ili barabara hiyo lianze kutumika.
" Kukamilika kwa sehemu hii sasa kunaifanya barabara yote toka Tabora hadi Kigoma km 413 kuwa ya lami na kuandika historia mpya kwa mikoa ya magharibi naTanzania kwa ujumla", amesema Eng. Kasekenya.
Amesema Serikali imedhamiria kuufungua mkoa wa Kigoma kwa barabara za lami kila upande, usafiri wa anga, reli na meli ili kuufanya mkoa huo kitovu cha uchumi wa mikoa ya magharibi na nchi jirani za Burundi na DRC.
Amesema barabara unganishi za Uvinza- Kasulu na Uvinza-Mishamo-Mpanda ziko katika hatua mbalimbali za maandalizi ya ujenzi wake.
" Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amejipanga kuufungua ukanda wa magharibi mwa nchi kimiundombinu ili kukuza uchumi", amesisitiza Naibu Waziri Kasekenya.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Dinah Mathamani ameishukuru Serikali kwa uwekezaji wa miundombinu ya kisasa mkoani Kigoma ambayo inachochea fursa za kilimo, biashara na uvuvi na hivyo kukuza uchumi.
Meneja wa TANROADS mkoa wa Kigoma Eng. Narcis Choma amemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya kuwa wamejipanga kuhakikisha daraja la Ruchugi na mzunguko wa Uvinza vinakamilishwa kabla ya mwisho wa mwezi Februari.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kasekenya amemtaka mkandarasi China Railway Construction Engineering Group anaejenga kiwanja cha ndege Kigoma kuhakikisha kinakamilika mwezi Mei mwaka huu.
Uboreshaji wa kiwanja cha ndege cha Kigoma ni muendelezo wa mkakati wa Serikali kuboresha viwanja vya ndege na usafiri wa anga nchini ambapo tayari viwanja vingine vya ndege vya Shinyanga, Tabora na Sumbawanga ujenzi wake uko katika hatua za mwisho.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Kigoma Rashid Chuwachuwa ameishukuru Serikali kwa upanuzi wa kiwanja cha ndege Kigoma na kuwaalika wawekezaji kuwahi fursa za uwekezaji mkoani humo.





No comments:
Post a Comment