Na Shua Ndereka
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amevitaka viwanda nchini kuwekeza na kuzalisha sukari kwa wingi kwani soko la sukari bado ni
kubwa katika bara la Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya kutembelea mabanda ya maonesho ya wakulima likiwemo banda la Bodi ya Sukari katika viwanja vya Mwl. Julius Nyerere vilivyopo halmashauri ya wilaya ya Morogoro, Waziri Kijaji amesema kuwa mazingira ya uwekezaji na biashara yameboreshwa.
Aidha amesema kuwa, kiwanda cha sukari cha Bagamoyo tayari kimeanza uzalishaji; navyo viwanda vya Mkurazi na Kilombero, hadi kufikia mwezi Septemba vitakuwa vimeanza uzalishaji kwa lengo la kuongeza wingi wa sukari nchini.
“...hatuna upungufu wa sukari nchini kwa sasa na hakuna eneo lolote ambalo sukari imeongezeka kwa kipindi cha miaka miwili tangu Rais wetu aingie madarakani, hivyo watanzania wawe na amani, bei ni ile ile kati ya 2,800 na 3,200 ukiuziwa sukari 4,000 toa taarifa sisi tushughulike...” amesema Kijaji.
Naye Mkulima kutoka Kilombero, Habibu Hashimu, ameeleza mafanikio mbalimbali waliyoyapata wakulima wa miwa; ambapo takwimu zinaonesha kuwa katika msimu wa mwaka 2013/2014 wakulima walivuna miwa tani laki sita elfu moja mia nane na tano (601,805) na wakati huo huo, wawekezaji walivuna tani milioni mbili laki moja na tisini na saba mia nane na sabini na saba (2,197,877).
Hali hiyo ya uzalishaji wa sukari imeongezeka maradufu kwa wakulima, ambapo katika msimu wa mwaka 2022/2023 uzalishaji umefikia milioni moja arobaini na sita elfu, mia nne themanini na tisa (1,046,489); jambo ambalo limepelekea mapato kufikia bilioni 102.72 kwa mwaka 2022/23, kutoka kuwa bilioni 36.43 mwaka 2013/14.
Mbali na mafanikio hayo, Hashimu ameiomba serikali kuwezesha miundombinu ya umwagiliaji ili kuongeza tija pamoja na kuwasaidia kuondoa changamoto ya miundombinu ya barabara na umeme katika eneo la Mkurazi.
“Sisi ni wakulima tunaojitahidi kulima miwa lakini tumekuwa na changamoto ya barabara na tumekuwa tukiwaomba TARURA kutusaidia kwa sababu tunalipa kodi; lakini wameeleza kwamba barabara zetu hazijasajiliwa hivyo tunaomba kupitia nafasi hii TARURA wakubali kuja kuzisajili barabara zetu ili tuweze kusafirisha miwa yetu kwa wakati” ameeleza Hashimu.
No comments:
Post a Comment