DKT.JAFO AWATAKA WANANCHI KUSHIRIKI KATIKA UHIFADHI WA TABAKA LA OZON - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, September 13, 2023

DKT.JAFO AWATAKA WANANCHI KUSHIRIKI KATIKA UHIFADHI WA TABAKA LA OZON


Na. Gideon Gregory, Dodoma.

Katika kuelekea siku ya tabaka la Ozon Septemba 16,2023 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo ametoa rai kwa kila mwananchi kushiriki katika uhifadhi wa tabaka hilo na kupunguza athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.

Waziri Dkt. Jafo ametoa rai hiyo leo Septemba 13,2023 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo ametaja mambo ya kuzingatia katika kufanikisha suala hilo.

"Moja ni kuepuka kuingiza nchini gesi zilizopigwa marufuku na vifaa vinavyotumia gesi jadidifu kama vile majokofu na viyoyozi vilivyotumika yaani ile mitumba au kuepuka kutupa ovyo vifaa vya kuzimia moto vyenye kemikali inayomomonyoa tabaka la Ozon au vyenye kusababisha ongezeko la joto duniani"amesema Dkt. Jafo.

Aidha, amesema tabaka la Ozon kazi yake ni kuchuja mionzi ya jua isifike katika uso wa dunia na kuongeza kuwa linapoharibika na kuruhusu mionzi hiyo kufika katika uso inasababisha kuongezeka kwa magonjwa mbalimbali ikiwemo saratani ya ngozi, mtoto wa jicho na upungufu wa kinga dhidi ya maradhi.

Amesema Tanzania ikiwa kama nchi mwanachama wa jumuiya ya kimataifa kwa mwaka 2022 serikali kupitia ofisi ya makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau mbalimbali waliadhimisha siku hiyo kwa kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa tabaka la Ozon na kuhamasisha matumizi ya kemikali ambazo ni rafiki kwa mazingira.

"Pia tulitoa mafunzo ya namna ya kudhibiti uingizaji wa kemikali nchini kwa maafisa wa idara ya serikali waliopo katika mipaka, mpaka wa Namanga pamoja na wanafunzi wa fani za viyoyozi katika chuo cha ufundi cha Arusha na mafundi wa viyoyozi na majokofu",amesema Dkt. Jafo.

Sambamba na hayo Waziri Dkt. Jafo ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya masuala ya mabadiriko ya tabia ya nchi Duniani (GCA).

No comments:

Post a Comment