Serikali imesema chini ya Uongozi thabiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inatatua changamoto mbalimbali za Vyuo vikuu nchini ikiwemo Chuo Kikuu huria kwa lengo la kufikia Uchumi wa kati.
Hayo yameelezwa leo Septemba 21,2023 Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa Umma na utawala Bora, Mhe. George Simbachawene wakati akizungumza na Uongozi wa Chuo hicho katika Mkutano ulioshirikisha Jumuiya ya waliosoma katika Chuo Kikuu huria na kutaka kuja na mbinu mpya za ufundishaji kwa wanavyuo namna ya kukabiliana na changamoto za maisha.
“Tujitahidi kutengeneza mfumo mzuri wa ujulishanaji, ndiyo maana huku serikalini tumefikiria vyuo vikuu viachwe vifanye majukumu yake vyenyewe ili kuweza kuandaa watu watakao weza kufanya vyema majukumu yao na kuweza kuliletea tija taifa letu la Tanzania,”amesema Mhe. Simbachawene.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wahitimu hao, Almas Maige ambaye ni Mbunge wa Tabora Mjini ameisistiza Jumuiya hiyo kudumisha Umoja huo katika kukitangaza Chuo hicho ndani na nje ya Nchi.
“Ni wajibu wa kila mwanachama kushiriki ipasavyo katika kutoa maoni na michango ya kifedha pia naomba kuahidi kila mwaka nitakuwa nachangia kiasi cha shilingi milioni 1, na kwasasa mpango mkakati wa Jumuiya hii ni kutumia rasilimali za chuo na kuendelea kubuni namna ya kuwasaidia vijana wengine,”amesema.
Aidha ametoa rai kwa wanachama kuja na mawazo mapya pamoja na mbinu za kuwafundisha wanafunzi namna ya kuwekeza na kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha.
Naye Rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho Felix Lugeiyamu amesema kuwa chuo hicho ni kama kidole gumba kwasasa kwani kimeweza kusomesha wanafunzi wengine katika vyuo mbalimbali hapa nchini.
Pia Rais huyo amemuomba Mhe. Simbachawene kuwaunga mkono katika mpango wao hupo wa kuwasaidia wanafunzi kusoma kwani suala hilo ni muhimu katika kuwasaidia vijana wengine kuweza kuifikia malengo yao.
“Serikali ya chuo huria ndiyo serikali pekee iliyofanikiwa kuwasomesha wanafunzi wengine vyuo, sasa naamini kupitia kwako tutapata ushirikiano mkubwa maana najua hili kwako halishindikani kutekelezwa,”amesema Rais Lugeiyamu.
No comments:
Post a Comment