KAMATI YAIPONGEZA SERIKALI KWA KUTENGA BAJETI KUBWA KWA AJILI YA MIRADI YA UMWAGILIAJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, October 7, 2023

KAMATI YAIPONGEZA SERIKALI KWA KUTENGA BAJETI KUBWA KWA AJILI YA MIRADI YA UMWAGILIAJI


Na Mwandishi wetu - Iringa

Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya viwanda, biashara, kilimo na mifugo Mhe. Mariam Ditopile, ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kutekeleza ahadi zake kwa vitendo, kwa kutenga bajeti kubwa kwaajili ya miradi ya umwagiliaji.

Mwenyekiti huyo pia ameipongeza serikali kwa kuhakikisha fedha zilizotengwa katika bajeti hiyo, zimetolewa na kusimamiwa vizuri katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati, ikiwemo skimu ya Mkombozi mkoani Iringa.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa skimu hiyo itakayokuwa na mashamba makubwa manne mara baada ya kukamilika, Mwenyekiti huyo amezitaka taasisi zote zinazoguswa na miradi ya umwagiliaji, kuwajibika kila mmoja kwa nafasi yake, ili kufikia malengo yaliyowekwa na serikali ya awamu ya sita ya kupanua wigo wa kilimo cha umwagiliaji nchini.


“Miradi ya maendeleo ilikuwa inatengewa fedha ndogo, lakini kwasasa wizara ya kilimo imetengewa karibu shilingi trilioni mmoja, hiyo ni hatua kubwa sana lazima tuipongeze, lakini sio kutenga tu lakini fedha zinakuja saiti mpaka mnaona hii mitambo ni kwasababu fedha zimekuja,kila mmoja wetu ahakikishe anawajibika fedha hizi zitimize malengo yaliyokusudiwa”


Kwa upande wake, naibu Waziri wa kilimo David Silinde,amesema rais Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amedhamiria kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo na kuwainua wakulima wadogo kwa kujenga miundombinu ya umwagiliaji ya kimkakati, ili walime mara mbili au zaidi kwa mwaka, hatimaye nchi ijitosheleze kwa chakula na kuuza kwa wingi nchi za nje.

“Kama kuna kipindi sisi kama nchi tumepata kiongozi anayehangaika na matatizo yetu ni Dkt Samia Suluhu Hassan.Tuendelee kumuunga mkono kwasababu anatuvusha na amedhamiria kumsaidia mwananchi wa kawaida.Kwahiyo,rai yangu kwa wananchi ni kuwa lengo la Mheshimiwa rais kwenye kilimo nini? Nikuongeza uhakika wa chakula nchini na hataki kusikia Tanzania tunalalamika njaa, amesema hataki kusikia”.

Naye Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw, Raymond Mndolwa, ametaja manufaa yatakayopatikana, katika kupitia mradi wa Skimu ya Mkombozi kuwa ni Pamoja na uzalishaji mkubwa wa zao la mpunga,utakaochagiza maendeleo katika sekta mbalimbali wakiwemo wakulima, wafanyabiashara na taifa kwa ujumla.

Aidha mjumbe wa kamati hiyo Mhe, Yahya Khamis, mbunge kutoka Zanzibar, amewaasa wakazi wa vijiji vitakavyonufaika na mradi huo kumshukuru Rais Dkt, Samia, kwa kuwaletea neema ya kilimo cha uhakika, huku akitoa ushuhuda namna yeye mwenyewe anavyonufaika na shughuli ya kilimo cha umwagiliaji katika skimu anazolima.

Skimu ya Mkombozi inajengwa na kampuni mbili za Confix na CRJE kwa gharama ya shilingi Bilioni 55, na ambayo inajumla ya wanufaika 13,000 watakaolima katika skimu hiyo mara ujenzi utakapo kamilika mwezi February 2024.

No comments:

Post a Comment