Na WMJJWM, Ruvuma
Serikali mkoani Ruvuma imewataka wanaume kuvunja ukimya dhidi ya vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa kwa baadhi ya wanaume wanao kumbana na madhila hayo.
Kauli hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa huo Jumanne Mankhoo wakati wa mafunzo ya siku moja yaliyowahusisha waratibu wa madawati ya jinsia kwenye maeneo ya Umma Oktoba 11, 2023.
“Ndugu viongozi na wataalam, Wizara imetoa mwongozo huu kwa lengo la kuhakikisha ukatili wa aina zote unadhibitiwa na kutokomezwa kabisa, ukiusoma mwongozo huu utaona kundi la wanawake na watoto wamekuwa wahanga wakuu wa vitendo vya ukatili, lakini kuna wanaume pia wanaofanyiwa ukatili. Hivyo niwaombe mvunje ukimya” amesema Mwankoo.
Mwankhoo amesema matukio mengi ambayo yamekuwa yakiwatokea wanaume yamesababishwa na wao kukaa kimya huku akitolea mfano wa askari Polisi aliyejikatili maisha muda mfupi baada ya kuingia kazini kwake eneo la Ofisi ya Mkoa huo siku chache zilizopita mkoani hapo.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Rennie Gondwe amesema tayari waratibu 215 wa awamu ya kwanza wamefikiwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Mwanza, Geita na Shinyanga.
“Baada ya kupata mafanikio kwenye awamu ya kwanza, ambapo tayari yamefunguliwa madawati 104, tuliona ni vema tukatanua wigo hivyo katika awamu hii ya pili, tulianza na mikoa ya Morogoro, Dar Es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara na sasa mkoa wa Ruvuma ambapo lengo ni kuwapatia mafunzo waratibu wasiopungua 220” amesema Gondwe.
Rennie amesema, ana imani baada ya mafunzo hayo waratibu hao wataanzisha na kuendesha madawati kama ilivyokuwa kwa mikoa ya awamu ya kwanza.
Kuanzishwa kwa Dawati la kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo ya umma kutawajengea uwezo Viongozi/ Kamati zilizopo wakati wa kushughulikia mashauri ya vitendo vya ukatili kwenye maeneo ya umma na kuweka utaratibu unaofaa wa kutoa taarifa na kushughulikia mashauri ya vitendo vya ukatili ndani ya maeneo ya umma.
No comments:
Post a Comment