JITOKEZENI KATIKA MIKUTANO YA HADHARA KUTANGAZA KAZI ZENU - MPANJU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, November 23, 2023

JITOKEZENI KATIKA MIKUTANO YA HADHARA KUTANGAZA KAZI ZENU - MPANJU


Na WMJJWM Arusha

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amewasisitiza Maafisa Maendeleo ya Jamii kujitokeza katika mikutano ya hadhara hasa ya viongozi wa kisiasa ili wanadi kazi zao kwa wananchi ili zifahamike zaidi.


Wakili Mpanju ameyasema hayo Novemba 22, 2023 jijini Arusha, wakati wa kufunga kongamano la siku tatu la Maafisa Maendeleo ya Jamii.


Amewahimiza Maafisa hao kutumia ushauri na mawazo waliyopata kwenye kongamano hilo kutoka kwa viongozi wao wenye uzoefu kwenye sekta hiyo ili kuboresha utendaji wa kazi zao na maisha ya wananchi.



“Mkitumia vyema maarifa mliyopata mtaweza kuwashirikisha wanajamii fursa zilizopo katika maeneo yao lakini inabidi mkae kwanza na muuelewe Mpango Kazi wa Taifa wa Maafisa Maendeleo ya Jamii kusimamia na Kuhamasisha Maendeleo wa mwaka 1996” amesema Wakili Mpanju.


Vilevile Wakili Mpanju amewasisitiza kuhakikisha wanawekeza katika utafiti wa fursa zilizopo katika maeneo yao ili kuwainua wananchi kiuchumi kwa kutumia fursa zilizopo ikiwemo kuimarisha Majukwaa ya kiuchumi yaliyopo vijijini.


Naye rais wa Chama cha Maafisa Maendeleo ya Jamii (CODEPATA),Victor Kabuje ameishukuru Serikali kwa niaba ya Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini na kuahidi kuwa ushauri, mawazo na maagizo waliyoyapata kutoka kwa viongozi hao yanawasaidia kuleta tija na mabadiliko katika utekelezaji wa majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.


Baadhi ya maazimio yaliyofikiwa katika Kongamano hilo ni pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum pamoja na Ofisi ya Rais- TAMISEMI kushauri mamlaka miradi yote ya kimaendeleo iwahusishe Maafisa Maendeleo ya Jamii katika ngazi zote lakini pia kuweka chapa ya kazi za maendeleo ya Jamii ili kuweza kuzitangaza katika vyombo vya habari ili wananchi wafahamu kazi kubwa wanayoifanya.

No comments:

Post a Comment