Na WMJJWM - Mbeya
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii kutekeleza majukumu yao kwa viwango, weledi na utaalam ili kuinua hali ya maisha ya watu waishio katika mazingira magumu ikiwa ni moja ya njia za kuleta maendeleo nchini.
Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la Ustawi wa Jamii na Mkutano Mkuu wa Chama cha Wataalam wa Ustawi wa Jamii Novemba 14, 2023 jijini Mbeya.
Dkt. Tulia amewapongeza Maafisa Ustawi wa Jamii kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na wanajamii bila kujali itikadi, dini na makabila yao hali ambayo imepelekea kuwaunganisha wananchi zaidi na kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake .
“Tanzania ni Nchi yenye watu wa makabila, fikra, dini, jinsi na tamaduni mbalimbali na tofauti hizi ni za thamani hivyo zapaswa kuheshimiwa na kila mtu ili kujenga jamii yenye amani, umoja na maendeleo na ni imani yangu kuwa Umoja wa Maafisa Ustawi wa Jamii Tanzania (TASWO) una uwezo wa kuendelea kuelimisha wanajamii juu ya kuheshimi tofauti hizi,” amesema Dkt. Tulia.
Aidha Dkt.Tulia amesema Serikali kupitia Wizara zake na Idara ya Ustawi wa Jamii imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Maafisa Ustawi wa Jamii wanafanya kazi katika mazingira salama kwa kuunda Sera, Sheria na Miongozo inayofaa.
“Natambua kiu yenu kubwa ni kuona jinsi gani Bunge litahimiza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kuharakisha uundwaji wa Sheria ya Ustawi wa Jamii ambayo itawezesha uwepo wa Baraza la Taaluma lenye udhibiti kwa watoa huduma wa Ustawi wa Jamii, katika hili nipende kuwahakikishia kuwa Bunge linaona nia na dhamira ya Serikali na mchakato huu unaenda kuisha kabla ya 2025,” amesema Dkt. Tulia.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa TASWO Salma Kundi, wakati akiwasilisha risala ameomba kuharakishwa kwa mchakato wa Sheria ya Ustawi wa Jamii itakayosaidia kuundwa kwa Baraza litakalosimamia ueledi kwenye taaluma ya Ustawi wa Jamii.
Kundi pia ameishauri Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii iendelee kufanya ziara za mara kwa mara za kikazi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuchunguza huduma za ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii, lakini pia kujionea hali halisi ya utoaji huduma za ustawi wa jamii kwenye halimashauri zetu na kuishauri Serikali ufumbuzi wa changamoto zilizopo.
No comments:
Post a Comment