Na Mwandishi Wetu Mkuranga,Pwani
CHUO kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), kimetoa Mafunzo ya mfumo wa akili bandia kwa afya ya mimea kwa baadhi ya wakulima wa Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani yenye lengo la kusaidia kufuatilia njia bora za kukabiliana na magonjwa ya mimea.
Mafunzo hayo ya Mradi wa kutengeneza mfumo huo una matarajio kuasaidia kufuatilia, kutabiri na kupendekeza njia bora za kukabiliana na magonjwa yanayosumbua mimea.
Dkt. Michael Mahenge kutoka SUA amesema mradi huo unafanywa kwa kushirikiana na mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali ambayo ni shirika linalokabiliana na viumbe viharibifu (TPHPA) na (RECODA) shirika linalojishughulisha na kuweka daraja la Teknolojia ili ziweze kuwafikia wakulima hasa wale wadogo kwa urahisi itakayowezesha kuendelea sehemu mbalimbali kwa kilimo chenye tija kwa kutumia mfumo wa jitihada shirikishi za kuleta mageuzi ya kilimo vijijini.
Dkt. Mahenge amesema lengo la Mradi huu ni kutatua changamoto za magonjwa ya mimea kwa kutumia teknolojia mbalimbali zikiwemo za akili bandia.
Amesema upatatikanaji wa taarifa na picha za majani ya mimea ili kuweza kuzitafsiri kupitia akili bandia kupata taarifa sahihi zitakazomsaidia mkulima hasa katika kukabiliana na mazao hayo, amesema atatumia teknolojia ya ndege zisizotumia rubani (Drones), simu janja na kamera za kidijitali katika mashamba ya kuanzia hekari tatu mpaka mia moja (100).
Aidha Dkt. Mahenge amesema anaishukuru Serikali kupitia COSTECH kwa kuendelea kufadhili miradi katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo ambapo amesema teknolojia hii itamsaidia mkulima kufuatilia afya ya mmea tangu wakati wa kupanda mpaka kuvuna ambapo itamwezesha namna ya kukusanya taarifa shambani kwa siku au wiki itategemea na jinsi alivyopanga.
Vilevile mfumo huo unalenga kuwaleta wadau wa kilimo pamoja ili kuhakikisha kilimo kinachofanywa kinaleta tija kwa wakulima wadogo wa kati na wa juu.
Aidha mfumo huo unalenga kwenye mazao ya kimkakati yanayotumika kwa kilimo kama vile maharage, mpunga, mahindi na muhogo ambapo kwa Wilaya ya Mkuranga wanaangalia taarifa za zao la muhogo na mahindi.
Kwa upande wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia Mfuko wa Taifa wa kuendeleza Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MTUSATE) imefadhili jumla ya miradi saba (7) inayotumia akili bandia ili kutatua changamoto katika Afya, kilimo, Elimu na masuala ya manunuzi. Amesema meneja wa MTUSATE Dkt. Beatrice Lyimo
Dkt. Lyimo amesema Mradi huo ambao unatatua changamoto ya Afya ya mmea ni moja kati ya miradi 7 iliofadhiliwa na COSTECH kwa kushirikiana na shirika la Maendeleo na Utafiti Canada na jumla ya shilingi milioni 150 zimetolewa kwaajili ya Mradi huu kwa matarajio ya kupata taarifa za changamoto za magonjwa ya mimea katika mazao manne yalichaguliwa zitapatikana kwa urahisi.
No comments:
Post a Comment