"RUSHWA CHANZO MIRADI KUJENGWA CHINI YA KIWANGO"- DKT. BULAMILE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, January 27, 2024

"RUSHWA CHANZO MIRADI KUJENGWA CHINI YA KIWANGO"- DKT. BULAMILE


Na Okuly Julius-Dodoma

Vitendo vya rushwa kwenye sekta ya ujenzi imeelezwa kuwa sababu ya miradi mingi ya barabara kujengwa chini ya kiwango na kuleta hasara kwa serikali.

Kauli hiyo imetolewa leo Januari 27,2023 Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Dkt. Ludigija Bulamile wakati akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa 10 wa bodi hiyo.

Dkt. Bulamile amesema kuna miradi mingi nchini ambayo imejengwa kwa kutumia fedha za walipa kodi wa Tanzania lakini haijadumu kutokana na kujengwa chini ya kiwango.

Amesema rushwa imesababisha fedha za kujenga kilomita moja ya barabara kutumika kujenga kilomita 20 ambazo baada ya muda mfupi zinaharibika kutokana na kujengwa chini ya kiwango.

“Kuna barabara ambazo zikikamilika zinakuwa ni nzuri lakini baada ya muda kidogo hasa wakati wa mvua unakuta hiyo barabara haipo imeshafagiliwa na maji, yote haya ni matokeo ya kutoa rushwa kwenye miradi ya ujenzi,” amesema Dk Bulamile na kuongeza kuwa,

“Ukikutana na mhandisi aliyejenga hiyo barabara na kumuuliza kimetokea nini anakujibu kuwa baada ya kupata tenda madiwani wamenifuata na kudai niwape asilimia kumi ya gharama za mradi… sasa hapo atapata wapi tena pesa za kukamilisha mradi huo?”

Amesema kutokana na kukithiri kwa vitendo vya rushwa kwenye sekta ya ujenzi ndiyo maana serikali iliamua kuanzisha wakala wa Barabara za Vijijini (TARURA) kwani iliona fedha nyingi zinatumwa kwenye Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa barabara lakini matokeo yalikuwa hayaonekani.

Amewataka wabunifu majengo hao kufanyakazi kwa uadilifu ili kulinda taaluma yao na kujiepusha na vuitendo vya rushwa ambavyo vinaigharimu serikali fedha nyingi.

Aidha amewataka kutembelea miradi mbalimbali ya kiserikali inayotekelezwa nchini ili kuona mapungufu yaliyopo na waweze kutoa ushauri utakaolisaidia Taifa.


Kwa upande wake Msajili wa Bodi hiyo, Edwin Nnunduma amewataka wabunifu majengo hao kuomba tenda kwenye miradi mbalimbali ya kitaifa inayoendelea nchini ili waweze kujiongezea mapato.

Amesema miradi mingi inayojengwa nchini haijapata michoro inayotakiwa na ndiyo maana kuna baadhi ya maeneo mvua ikinyesha kunakuwa hakuna mifereji ya kupitisha maji kutokana na michoro ya miradi kukosewa.

Msajili huyo ameiomba serikali kuharakisha sheria ya majengo ambayo itakapokamilika itawasaidia wabunifu majengo hao kushiriki kwenye ujenzi wa miradi yote ya kitaifa nchini kitu ambacho hawawezi kufanya kwa sasa kutokana na kutokuwepo kwa sheria hiyo.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi wa migodi, nishati na ujenzi Tanzania (TAMICO) tawi la AQRB, Mlezi Makuka amewataka wafanyakazi hao kufanya kazi kwa bidii ili waweze kuliletea Taifa mafanikio na wao kujipatia kipato.

Amesema kila mmoja akitimiza wajibu wake suala la kuongezewa kima cha chini cha mshahara kitakuwa rahisi kwa kuwa tija itaonekana hivyo hata wakidai nyongeza ya mshahara haitakuwa tatizo.

No comments:

Post a Comment