Imeelezwa kuwa ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Korea Kusini umechochea kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini ikiwemo mradi wa kimkakati wa daraja la Tanzanite lililojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Korea Kusini kupitia mfuko wa ushirikiano wa maendeleo ya kiuchumi (Economic Development Cooperation Fund -EDCF)
Hayo yamebainishwa leo, Ijumaa Januari 26.2024 Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano yaliyohusisha Ofisi ya Waziri Mkuu na National Agency for Adminstrative City Constraction and Heerim Architects and Planners ya Nchini Korea Kusini ambapo pamoja na mambo mengine amesema kusainiwa kwa makubaliano hayo kunaweka msingi imara wa Biashara na Uwekezaji baina ya Nchi hizo mbili huku miradi mingi zaidi ikitarajiwa kurekelezwa Nchini hususani Jijini Dodoma ambako ni Makao makuu ya Tanzania
Amesema kupitia kusainiwa kwa hati hizo Tanzania itanufaika na teknolojia ya kisasa ya usanifu na ujenzi wa majengo na miundombinu mingine itayopendezesha mji mkuu Dodoma, sambamba na kupatikana kwa fursa mpya za ushirikiano na makampuni ambayo yana uzoefu mkubwa wa usanifu na ujenzi hususani wa majengo katika miji na majiji makubwa
Waziri Jenista amesisitiza kuwa maendeleo ya Jiji la Dodoma yanahitaji uwekezaji mkubwa katika majengo, maeneo ya mapumziko, mazingira, miundombinu ya mawasiliano na maeneo mengine ya kuvutia hivyo ili kufikia lengo hilo Serikali inapaswa kushirikiana kikamilifu na sekta binafsi ili kufikia maendeleo hayo
"Akiwa Korea Kusini Mheshimiwa Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) aliitembelea National Agency for Administrative City Construction, taasisi hii ni wakala wa kitaifa nchini Korea Kusini inayosimamia na kuendeleza ujenzi wa jiji la Sejong nchini humo, kimsingi jiji la Sejong limejengwa kwa mandhari nzuri na ya kuvutia sana, muonekano wake wa kuvutia ulimfanya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa niaba ya Serikali ya Tanzania kumkaribisha Mtendaji Mkuu wa taasisi hii Nchini Tanzania ili kubadilishana uzoefu na viongozi wa taasisi zinazofanana na hizi hapa kwetu Tanzania" -Waziri Jenista
No comments:
Post a Comment