Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye, ametoa ufafanuzi jinsi huduma za mawasiliano zilivyokuwa gharama kuanzia ujenzi hadi uendeshaji.
Mhe. Nape Nnauye ameyasema hayo leo Januari 24.2024 jijini Dodoma katika hafla ya uzinduzi wa mpango wa elimu kwa umma kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano vijijini.
Amesema idara ya 61 ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inaeleza kwa kipindi cha miaka mitano sekta ya mawasiliano imejikita zaidi katika kuimarisha ubora wa mawasiliano nchini na kuhakikisha wigo wa mawasiliano unaongezeka na kuwafikia wananchi bila kujali umbali.
“Huduma za mawasiliano ni gharama, gharama kwenye kujenga ile miundo mbinu, mnara mmoja wa mawasiliano unagharimu karibia milioni 350 kuuendesha kwa mwezi mmoja ukitumia mafuta haya ya dizeli ni milioni 1 na laki 8, ukionganisha kwa umeme inashuka kidogo inakuja laki 4 na bado gharama zengine za ulinzi na mengineyo na kuupeleka kwenye viijiji ambao watumiaji wake pengine wanatumiana mesej na kupigiana simu wakati kwa kubania bania ki biashara haulipi.”
“Rais Samia kupitia mfuko wa mawasiliano UCSA alichofanya ni kusema kwa kuwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi imetuagiza kila alipo mwananch kila mtu afikiwe, sasa atafikiwaje ndio ikatengwa fedha ili tuwape ruzuku makampuni ya simu yapunguze gharama zao za kupeleka mnara kwenye kijiji ambacho hakina mvuto wa kibiashara, tunaongeza ela juu yake ili mnara ufike,”amesema Nnauye.
Kadhalika alisema tarehe 13,3,2023 Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dtk. Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya utiaji saini wa mikataba wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano pamoja na utiaji saini wa uboreshaji wa minara na kuongeza nguvu minara 304 kutoka teknolojia ya 2G na kwenda 3G na kuendelea.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema kuwa serikali imetumia bilioni 6 kwa mkoa wa Dodoma katika kuimarisha upatikanaji wa habari na mawasiliano kwa namna ya pekee kupitia minara hiyo katika vijiji, kata pamoja na manufaa kwa watu.
“Kwa mkoa wa Dodoma kupitia UCSAF tulifanikiwa kupata minara 77 ambayo zikiwa kata 68, vijiji 202 na imeweza kufikia watu laki 750 hiyo ambayo ilikuwa zaidi ya bilioni 11 lakini kupitia minara 758 ambayo leo inaenda kuzinduliwa namna ya utekelezaji wake sisi mkoa wa Dodoma tumefaidika na minara 36 ambayo pia kata 36, vijiji 56 na watu 402,000 watafaidika kwa mawasiliano kwa uwepo wa minara hii na ambapo pia imetumia jumla ya shilingi bilioni 6 kwa mkoa wa Dodoma.”amesema Senyamule.
Kwa upande wake afisa mtendaji Mkuu wa UCSAF Justina Mashiba amesema kuwa kwa muujibu wa sensa ya mwaka 20/22 karibia asilimia 68 ya watanzania wanaishi vijijini na asilimia ndogo iliyobaki wanaishi maeneo mjini hivyo serikali kwa kupitia Bunge waliunda sheria na kuanzisha taasisi ya mfuko wa mawasiliano kwa wote UCSAF ili kushirikiana na watoa huduma kupeleka huduma hizo.
“Tunatarajia kwenda mkoa kwa mkoa kwasababu mradi huu ni mradi mkubwa ambapo serikali imewekeza fedha zaidi ya bilioni 326 ambazo serikali inatoa kama ruzuku lakini pia watoa huduma za mawasiliano wanachangia kuhakikisha kuwa watanzania wanaoishi katika maeneo ya vijijini wanapata huduma za mawasiliano.”amesema Mashimba.
Mhe. Nape Nnauye alimalizia kwa kusisitiza utumiaji mzuri wa mitandao kwa manufaa chanya pamoja kuhimiza wazazi kuwa makini na watoto wao wanapotumia mitandao pamoja na umuhimu wa kila wananchi kulinda miundombinu ya mawasiliano itakayojengwa kwani huduma ya mawasiliano ni fursa katika elimu, kilimo, biashara pamoja na afya.
No comments:
Post a Comment