Na Carlos Claudio, OKULY BLOG, DODOMA
Serikali haitamvumilia mtoa huduma yeyote ambaye atashindwa kusimamia usalama wa vifaa tiba vinavyopelekwa kwa ajili ya kuboresha huduma za afya nchini.
Pia imewataka watoa huduma kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi ili kuleta thamani ya uwekezaji wa Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya nchini.
Akizungumza na Waganga wafawidhi wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za Afya ngazi ya msingi nchini leo Februari 13,2024 Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Mhe Dkt Festo Dugange amesema serikali haitamvumilia mtoa huduma yeyote ambaye atashindwa kusimamia usalama wa vifaa tiba vinavyopelekwa kwa ajili ya kuboresha huduma za afya nchini.
“Ni Jukumu lenu Waganga wafawidhi kuhakikisha mnasimamia kwa ufanisi mkubwa vifaa tiba na kuvitumia kwa matumizi sahihi na si vinginevyo” amesema Dkt. Dugange
Amewataka waganga hao kuimarisha ushirikiano wao na watumishi wanao waongoza ili kuleta ubora wa huduma katika kuwahudumia wananchi.
Hata hivyo amesema Serikali itatenga bajeti katika kila mwaka wa fedha kwa ajili ya kununua mafuta kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino).
“Tuzingatie utoaji wa huduma kwa watu wenye mahitaji maalum hasa Albino, tengeni bajeti ya mahitaji maalum kulingana na mahitai yao, utengaji wa fedha kwaajili ya mafuta maalumu kwa wenye ualibino ni maelekezo ya serikali na ni ya muhimu” amesema Dkt. Dugange
Amebainisha kuwa katika kipindi Cha miaka mitatu Halmashauri 47 tu zilitenga fedha kwaajili ya mafuta ya watu wenye ulemavu wa ngozi, (Albino) hivyo ni vyema katika utoaji wa huduma kuwatambua ili wapate mafuta hayo yatakayowakinga na vitu mbalimbali.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amewataka waganga hao kupita maeneo ya huduma kuangalia wananchi wanavyopata huduma ikiwemo kuangalia muda wanaokaa na kusubiri kupata huduma badala ya kukaa ofisini.
“Nasisitiza daktari, muuguzi, mtaalamu wa maabara na wengine wote piteni mawodini na kufungua majalada ya wagonjwa kuona huduma gani wagonjwa wamepatiwa tangu wamefika hospitali, je wanapata dawa na vipimo vilivyoandikwa, watumishi wapo na kama wanawajibika”. Amesisitiza Dkt. Magembe.
Ameongeza kwa kusema kuwa watumishi wasijifungie maofisini tu, bali watumie ujuzi wao kama viongozi wa vituo kuhakikisha wanatoa Huduma bora kwa wananchi ili kuleta thamani ya uwekezaji wa Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya nchini.
Akiongea kwa niaba ya Waganga wafawidhi hao Mwenyekiti wa Waganga wafawidhi wa vituo vya huduma za afya Msingi Tanzania bara you Dkt. Florence Hilari ,amesema kuwa watazingatia maelekezo waliyopewa na kuyafanyia kazi kwa ufanisi na hatimaye kutoa Huduma bora.
No comments:
Post a Comment