Na. Asila Twaha, Babati
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeielekeza Ofisi ya Rais - TAMISEMI Kufanya, ufuatiliaji na uchunguzi wa fedha walizopeleka kutekeleza miradi katika mkoa wa Manyara hasa katika miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi na kusema kuwa Kamati haijaridhishwa na ubora wa miradi na kasi ya miradi.
Kauli hiyo imetolewa na Kamati tarehe 18 Machi, 2024 ikiwa ni muendelezo wa ziara ya kikazi katika mkoa wa Manyara kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na Babati.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Ester Bulaya (Mb) akieleza kutokufuraishwa na usimamizi, ufuatiliaji, ufanisi na ubora wa miradi, kutokukamilika kwa wakati katika mkoa huo.
Akielezea jinsi Serikali inavyotafuta fedha za uwekezaji wa miradi ya maendeleo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili ziweze kuendesha shughuli zake ikiwa ni pamoja na kuwahudumia wananchi wa maeneo husika lakini amesema wapo baadhi ya watumishi wanakosa uadilifu na uaminifu na kufanya fedha hizo kama za bure ilihali zinatoka katika kodi za wananchi.
Akitolea mfano wa kutokukamilika kwa mradi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Babati na Nyumba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuwa fedha zilishatolewa na hadi sasa miradi hiyo haijakamilika na bado Halmashauri imeomba kuongezewa fedha za kumaliza miradi hiyo.
Amesema tabia iliyozoeleka kwa baadhi ya Halmashauri zikipewa fedha za miradi na zikimaliza fedha hizo husema zitaomba Ofisi ya Rais TAMISEMI na zitaongezewa sio sawa kwani tabia hiyo inawalemeza na kuzitaka Halmashauri kuangalia lengo la kuanzishwa kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuwataka wajue kuwa kwa vitu vidogo lazima wajitegemee.
"haiwezekani Halmashauri inakusanya mapato zaidi ya bilioni 3 lakini inashindwa kuchangia kuendeleza miradi ya maendeleo katika Halmashauri yake hata milioni 30 tu ikipungukiwa mradi hauendelei inaomba TAMISEMI iwaletee hii haiwezekani na haikubaliki” amesisitiza Mhe. Bulaya
Kwa upande kwa Mhe. Ally Makoa (Mb) akisoma mapendekezo kwa niaba ya Kamati imeitaka Ofisi ya Rais – TAMISEMI kufuatilia na kujiridhisha kabla haijaidhinisha fedha wanazoombwa za nyongeza kutoka Halmashauri kumalizia miradi na badala yake wafanye ufuatiliaji kwanza.
Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais -TAMISEMI Dkt. Charles Msonde amesema TAMISEMI itaendelea kushirikiana na Kamati kwa kuwa wanayoyaelekeza ni kwa maslahi ya wananchi na nchi ni yao ambapo amewasisitiza Watendaji wa Halmashauri kuwa waadilifu na wafuatiliji wa miradi ya maendeleo kwa sababu wameaminiwa na Serikali.
No comments:
Post a Comment