MAAGIZO YA KATIBU MKUU MPYA WIZARA YA MAJI KWA MAMLAKA ZA MAJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 18, 2024

MAAGIZO YA KATIBU MKUU MPYA WIZARA YA MAJI KWA MAMLAKA ZA MAJI

Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri , akizungumza leo Machi 18 ,2024 jijini Dodoma Wakati wa Uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa kipindi cha Mwaka 2022/2023.
Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dkt. James Andilile , akizungumza leo Machi 18 ,2024 jijini Dodoma Wakati wa Uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa kipindi cha Mwaka 2022/2023.

Na Okuly Julius Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri ameziagiza Mamlaka za Maji za Mikoa , kushirikiana na Halmashauri zote za Wilaya kuhamasisha uvunaji wa maji ya mvua katika ngazi zote hasa katika kipindi hiki ambapo mvua zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi.


Amesema mvua hizo zimeleta madhara katika baadhi ya maeneo, hivyo basi, endapo maji yake yatavunwa yatapunguza kama siyo kuondoa athari zake na pia kutaiwezesha nchi na wananchi kuwa na akiba ya maji ambayo yatasaidia kipindi cha ukame.

Mhandisi Mwajuma ametoa maagizo hayo leo Machi 18 ,2024 jijini Dodoma Wakati wa Uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa kipindi cha Mwaka 2022/2023.

“ Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya mwaka 2030 na hususan Lengo Namba 6 linaeleza umuhimu wa Majisafi na Usafi wa Mazingira. Lengo hili linasisitiza kuhakikisha uwepo na usimamizi endelevu wa maji na usafi wa mazingira kwa wote ikiwa ni pamoja na watu wote kuwa na uhakika wa upatikanaji wa majisafi na salama ya kunywa kwa bei nafuu ifikapo mwaka 2030,”

Na kuongeza kuwa “ EWURA inategemewa katika utekelezaji wa lengo hili ukiacha wadau wengine kwani ndiyo iliyopewa dhamana ya udhibiti wa sekta hii nyeti. Tumeshuhudia tangu EWURA ianze kuzisimamia mamlaka za maji nchini, kumekuwa na maboresho ya utendaji wa mamlaka hizi. Ni kwa msingi huu, naendelea kuipongeza EWURA na kuitaka iendelee kufanya kazi ya udhibiti kwa uwazi, ufanisi, weledi na tija kama ilivyoainishwa kwenye dhamira ya kuanzishwa kwake ili pia kumsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza Ilani,’’ amesema Mhandisi Mwajuma



Amesema kuwa Taarifa hiyo inaonesha kuimarika kwa baadhi ya viashiria vya utendaji kwenye Mamlaka za Maji ikilinganishwa na Mwaka wa Fedha 2021/22 na kuzipongeza mamlaka za maji kwa kuendelea kuboresha utendaji kazi wao katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Pia amezitaka Mamlaka za Maji kuzingatia miongozo mbalimbali ya kudhibiti upotevu wa maji ambayo hutolewa na EWURA kama vile Mwongozo wa kupunguza upotevu wa maji wa mwaka 2021 ambao unazitaka Mamlaka za Maji kuandaa mizania ya kupima viwango vya upotevu wa maji kwa mujibu wa mwongozo wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wataalam wa Maji (IWA).

“Pamoja na kumairika kwa baadhi ya viashiria vya utendaji wa mamlaka za maji ambavyo baadhi nimevitaja hapo awali, nimesikitishwa na kuendelea kuzorota kwa baadhi ya viashiria hivyo pamoja na kushindwa kufikiwa kwa malengo ambayo mamlaka hizo zilijiwekea,

Na kuongeza kuwa “taarifa inaonesha kuwa, upotevu wa maji dhidi ya kiwango cha maji kinachozalishwa umeongezeka kutoka asilimia 35.5 mwaka 2021/22 hadi kufikia asilimia 37.2 mwaka 2022/23. Ndugu zangu hii haikubaliki hata kidogo. Sote tunajua kiwango cha upotevu wa maji kinachokubalika ni chini ya asilimia 20. Ni lazima mamlaka za maji ziweke na kutekeleza mikakati ya kuhakikisha zinapunguza kiwango cha upotevu wa maji,” ameeleza Mhandisi Mwajuma

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dkt. James Andilile amesema taarifa iliyozinduliwa leo ni ya 15 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo miaka 18 iliyopita na inahusisha uchambuzi wa utendaji wa mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira 85 zikiwemo; mamlaka 25 za mikoa, saba (7) za miradi ya kitaifa, 47 za wilaya na Sita (6) za miji midogo.


Dkt.Andilile amesema kuwa kwa ujumla, utendaji wa mamlaka za maji na usafi wa mazingira umeendelea kuimarika ambapo kwa mwaka 2022/23, Mamlaka za Maji 78 kati ya 85 zilipata alama kuanzia wastani hadi vizuri sana katika utendaji wa ujumla ikilinganishwa na mamlaka 77 kati ya 90 kwa mwaka 2021/22.


Ameyataja Maeneo yaliyoimarika kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na mwaka 2021/22 kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha maji yaliyozalishwa kutoka mita za ujazo milioni 393 hadi 400 sawa na asilimia 1.8 , kuimarika kwa uwiano kati ya watumishi na wateja kutoka 4.2 hadi 3.8 kwa kila wateja 1000 , kuimarika kwa Uwiano wa maunganisho yaliyofungwa dira za maji kufikia asilimia 92 ikilinganishwa na asilimia 90 ,kuongezeka kwa kiwango cha ubora wa maji yanayosambazwa kwa wateja kutoka asilimia 91 hadi 94;

Maeneo mengine ni kuongezeka kwa wateja wa maji wa majisafi kutoka kutoka 1,385,485 hadi 1,532,362 sawa na asilimia 11 na kuongezeka kwa wateja wa mtandao wa uondoaji majitaka kutoka wateja 55,996 hadi wateja 56,899 sawa na asilimia 16.

“Nafahamu kuwa mafanikio hayo hayakuja bure. Naomba nitumie fursa hii kumpongeza na kumshukuru Mh. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wewe Mheshimiwa Waziri kwa usimamizi wako mahiri wa sekta ya maji kwa kufanya uwekezaji mkubwa kwa lengo la kumtua mama ndoo kichwani na kuimarisha ustawi wa watanzania wote, kwani maji ni UHAI.,” amesema Dkt. Andilile

Pia Uzinduzi huo umekwenda sambamba na utoaji wa tuzo mbalimbali Kwa Mamlaka zilizofanya vizuri huku zikigawanywa katika makundi Matatu tofauti kulingana na idadi ya wateja inayowahudumia ambapo kundi la kwanza ni Mamlaka za maji zenye wateja chini ya 5000, kundi la pili ni mamlaka za maji zenye wateja chini kati ya 5000 na 20,000 na kundi la Tatu ni mamlaka za maji zenye wateja zaidi ya 20,000.


MAMLAKA AMBAZO HAZIKUFANYA VIZURI KATIKA UTOAJI WA HUDUMA YA MAJISAFI KWA MWAKA 2022/23. MAMLAKA HIZO NI

SONGE iliyoshika nafasi ya 48 miongoni mwa mamlaka za maji 48 zenye wateja chini ya 5000.

“kundi la III la Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira”.

KOROGWE iliyoshika nafasi ya 18 miongoni mwa mamlaka za maji 18 zenye wateja chini kati ya 5000 na 20,000. “kundi la II la Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira”.

ROMBO iliyoshika nafasi ya 19 miongoni mwa mamlaka za maji 19 zenye wateja zaidi ya 20,000. “kundi la I la Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira”.

MAMLAKA ZA MAJI ZILIZOFANYA VIZURI ZAIDI KATIKA KUTOA HUDUMA

Mamlaka zilizofanya vizuri zaidi katika katika utoaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira, washindi katika Kundi la Kwanza yaani Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira za zenye wateja zaidi ya 20,000. Kundi hili lina jumla ya Mamlaka za Maji 19

TANGA imekuwa mshindi wa Tatu: Imezadiwa Cheti


MOSHI imekuwa mshindi wa Pili: Imezadiwa Cheti


IRINGA imekuwa mshindi wa Kwanza: Imezadiwa Ngao na Cheti

Washindi katika Kundi la Pili yaani Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira za zenye wateja zaidi kati ya 5,000 na 20,000. Kundi hili lina jumla ya Mamlaka za Maji 18

BUSEGA imekuwa mshindi wa Tatu: Imezadiwa Cheti

IGUNGA imekuwa mshindi wa Pili: Imezadiwa Cheti

NZEGA imekuwa mshindi wa Kwanza: Imezadiwa Ngao na Cheti

Washindi katika Kundi la Tatu yaani Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira za zenye wateja chini ya 5,000. Kundi hili lina jumla ya Mamlaka za Maji 48

LOLIONDO imekuwa mshindi wa Tatu: Imezadiwa Cheti

MASWA imekuwa mshindi wa Pili: Imezadiwa Cheti

BIHARAMULO imekuwa mshindi wa Kwanza: Imezadiwa Ngao na Cheti


MAMLAKA ZA MAJI ZILIZOFANYA VIZURI ZAIDI KATIKA KUFIKIA MALENGO YA KIUTENDAJI

Mamlaka zilizofanya vizuri zaidi katika kufikia malengo ya kiutendaji (performance targets) katika utoaji wa huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira naomba uzipatie cheti.

Washindi katika kundi la Kwanza

KASHWASA imekuwa mshindi wa Tatu

BABATI imekuwa mshindi wa Pili

TABORA imekuwa mshindi wa Kwanza


Washindi katika kundi la Pili. Hawa nao wanapata Cheti

MTWARA imekuwa mshindi wa Tatu

WANGING’OMBE imekuwa mshindi wa Pili

LINDI imekuwa mshindi wa Kwanza

Washindi katika kundi la Tatu. Hawa nao wanapata Cheti

TUNDUMA imekuwa mshindi wa Tatu
BIHARAMULO imekuwa mshindi wa Pili
MBINGA imekuwa mshindi wa Kwanza


MAMLAKA ZA MAJI ZILIZOFANYA VIZURI KATIKA KUWASILISHA TOZO YA UDHIBITI

Mamlaka za Maji zilizofanya vizuri katika uwasilishaji wa tozo ya udhibiti, naomba uzipatie cheti. Mamlaka hizi ni Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira;
Babati, Loliondo, Mbeya, Makambako, Itumba-Isongole, Orkesumet, Tukuyu, Turiani, Morogoro na Ruangwa

No comments:

Post a Comment