Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kikamilifu kuboresha na kufungua mawasiliano ya barabara na madaraja katika Mkoa wa Lindi ili kuchochea fursa za kiuchumi na kuboresha maendeleo ya wananchi.
Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi mara baada ya kufanya tathmini ya uharibifu wa miundombinu ya barabara na kukagua utekelezaji wa urejeshwaji wa barabara zilizoathirika na mvua na kuridhishwa na utekelezaji wake ambapo tayari barabara za Wilaya ya Liwale zimefunguka na Shughuli za kimaendeleo zinaendelea.
Bashungwa amesema Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi itatenga bajeti maalum kuhusu ukarabati wa barabara ya Liwale - Nangurukuru ili kuirudisha barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe kama ilivyokuwa awali na wananchi kuendelea kuitumia katika shughuli zao.
“Wana Liwale barabara hii ndiyo mnaoitegemea kiuchumi, baada ya kuifungua sasa ni kuitengea bajeti maalum ili iweze kupitika vipindi vyote na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji wa bidhaa kutoka mikoa jirani na katika bajeti ijayo 2024/25 tutaanza ujenzi wa kilometa 10 kwa kiwango cha lami”, amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa kazi ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara ya Nangurukuru - Liwale na barabara ya Liwale - Nachingwea katika maeneo korofi yote inaendelea vizuri ambapo kazi hiyo inatekelezwa na Wakandarasi watatu ili kuhakikisha zinakamilika kwa haraka zaidi na wananchi wanaendelea na huduma za kijamii.
Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inajipanga kujenga barabara ya Masasi-Nachingwea-Liwale na Ruangwa - Nachingwea kwa kiwango cha lami ili kutibu barabara hizo ambazo zimekuwa zikisumbua hasa vipindi vya mvua.
Nae, Mbunge wa jimbo la Liwale, Zuberi Kuchauka, amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwatuma Mawaziri na Wataalam kusimamia urejeshaji wa miundombinu ya barabara katika jimbo lake na sasa huduma zingine za kijamii zinaendelea.
No comments:
Post a Comment