BASHUNGWA AZITAKA TANROADS NA TARURA KUSHIRIKIANA KUFANYA TATHIMINI YA MIUNDOMBINU ILIYOATHIRIWA NA MVUA - OKULY BLOG

Breaking

Home Top Ad

TANGAZA NASI HAPA | PIGA 0785 364 965

Tuesday, April 30, 2024

BASHUNGWA AZITAKA TANROADS NA TARURA KUSHIRIKIANA KUFANYA TATHIMINI YA MIUNDOMBINU ILIYOATHIRIWA NA MVUA


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kushirikiana na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI kuunda timu za wataalam zitakazoshirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kufanya tathimini ya mtandao wa barabara pamoja na madaraja yaliyopata athari za mvua ili mvua zitakapokata matengenezo ya miundombinu iweze kuanzamara moja.

Bashungwa ametoa agizo hilo Aprili 30, 2024 Mkoani Dar es Salaam wakati akikagua barabara ya Mwaikibaki(Morocco-Africana) yenye urefu wa kilomita 11.7, ambayo inaenda kufanyiwa upanuzi wa barabara kuwa njia nne na Wakala ya Barabara (TANROADS) ikiwa ni kwa ajili ya kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji la Dar es Salaam.


“Nimemuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi amshirikishe Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoana Serikali za Mitaa - TAMISEMI kuunda ‘task force”ambayo itashirikiana na Mkoa wakubaliane mtandao wa barabara zote zilizopo TANROADS na TARURA ili baada ya mvua kumalizika zianze kufanyiwa marekebisho”, amesisitiza Waziri Bashungwa.

Bashungwa ameeleza kuwa lipo hitaji la TANROADS kushirikiana na TARURA kufanya uhakiki upya wa barabara zote na zile ambazo zitarudiwa kujengwa kwa ubunifu utakaoendana na mabadiliko ya tabia nchi ilikutunza barabara kwa muda mrefu.

Kuhusu upanuzi wa barabara ya Mwaikibaki (Morocco - Africana) yenye urefu wa kilometa 11.7, Waziri Bashungwa ameeleza kuwa katika barabara hiyo litatengwa eneo kwa ajili ya miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) ambapo hatua iliyopo hivi sasa nikumtafuta Mkandarasi wa barabara hiyo.

“Barabara hii ya Mwaikibaki ina vipande vitatu itakayoanzia Morocco kuelekea Africana kupitia Kawe ya Chini, Kawe - Lugalo na kipande kingine ni kile cha Mwalimu Nyerere cha kwenda Rose Garden vyote hivi vitajengwa kwa njia nne na tutatoa matoleo ya kujenga mabasi ya mwendo kasi ya BRT”, amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour kuangalia uwezekano wa kutengeneza barabara za mchepuo kwa ushirikiano wa TANROADS na TARURA zitakazounganishwa kutokea Daraja la Tanzanite na barabara ya Mwaikibaki ili kusaidia kupunguza adha ya msongamano wa magari nyakati za asubuhi na jioni.

Vilevile, Bashungwa amewaomba wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla kuacha tabia ya kufanya mifereji ya barabara kuwa dampo la takataka kwani kufanya hivyo kunasababisha maji kuhama na kuingia katika makazi ya watu pia kupita juu ya miundombinu ya barabara na madaraja yanayosababisha athari za miundombinu.

Hali kadhalika, Bashungwa ameelekeza TANROADS, TARURA na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), kuwachukulia hatua kali za kisheria Wakandarasi ambao hawazingatii afya na usalama wa wafanyakazi mahala pa kazi kama ambavyo inaonekana katika kazi mbalimbali za ujenzi vibarua kutokuwa na vifaa maalum vya kujikinga.

Kwa upande wake Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi John Mkumbo ameeleza kuwa usanifu wa barabara ya Mwaikibaki umefanywa na Kampuni ya Norplan ya Tanzania na kwa sasa barabara hiyo ina njia mbili ambayo imekuwa ikileta msongamano wa magari.

No comments:

Post a Comment

HABARI KUU KWA SASA

Wanahisa wa Benki ya CRDB waidhinisha Malipo ya Gawio la Shilingi Bilioni 130.6 kwa Mwaka wa Fedha wa 2023

Arusha 18 Mei 2024 - Wanahisa wa Benki ya CRDB wameidhinisha kwa kauli moja mapendekezo ya Bodi ya Wakurugenzi kuhusu malipo ya gawio la Shi...