Ashrack Miraji, Same Kilimanjaro.
Mkuu wa wilaya ya Same Mhe. Kasilda Mgeni ameishukuru Wizara ya Afya na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kuratibu na kusimamia vyema utoaji wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV) kwa mabinti ili kuwakinga na maambukizi ya virusi vinavyosababisha kansa hiyo.
Ametoa shukrani hizo wakati akizundua rasmi wiki ya chanjo Afrika yenye lengo la kufanya kampeni ya chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwenye wilaya ya Same ambapo alisema zoezi hilo limefanikishwa na Wizara ya Afya na OR-TAMISEMI.
“Tunazishukuru sana wizara hizi maana watumishi wake walio ngazi za wilaya na mikoa ndio wasimamizi na watekelezaji wakuu wa zoezi hili katika maeneo yao na wamekuwa wakifanya kazi zao kwa weledi mkubwa” alisema Mhe. Kasilda.
Ametoa wito kwa wazazi na walimu kuhakikisha kuwa mabinti wote wenye umri wa miaka 9-14 wanapata chanjo hiyo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwani takwimu zinaonyesha kuwa kila mwaka wanawake zaidi ya elfu kumi hugundulika kuwa na maambukizi ya saratani ya mlango wa kizazi na zaidi ya elfu sita hupoteza uhai sawa na asilimia 60%.
"Takwimu zinaonyesha kwa mwaka 2023 jumla ya wanawake 10,868 waligundulika kuambukizwa saratani ya mlango wa kizazi"
Mkuu huyo wa wilaya amesema chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi inawalinda mabinti kutopata saratani hiyo ambayo inamadhara mengi ikiwemo upungufu wa damu, kuharibu via vya uzazi na kupelekea mwanamke kushindwa kuendelea kuzaa, fistula na hata kupelekea kifo iwapo haitagundulika mapema na kutibiwa.
Awali akitoa taarifa fupi ya zoezi hilo mganga mkuu wa wilaya ya Same Dkt. Alex Alexander alisema zoezi hilo litafanyika kwa siku tano kuanzi April 22 -26 ambapo wilaya inatarajia kuchanja mabinti 3,768.
“Tupo katika maadhimisho ya wiki ya Chanjo Afrika ambayo hufanyika mwezi April kila mwaka na kwa mwaka huu kitaifa tumeamua kuchanja mabinti zetu ili kuwalinda na ugonjwa huu hatari”, alisema Dkt. Alexander.
Akizungumza katika hafla hiyo kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Same Dkt. Cainan Kiswaga amesema wilaya imejipanga vyema kuhakikisha kuwa mabinti wote wanaopaswa kuchanjwa wanapata chanjo ili kuwalinda na saratani hiyo.
Nae afisa afya wa mkoa wa Kilimanjaro Bw. Happinus Pilula amesema, "saratani ya mlango wa kizazi ndio saratani inayoongoza kwa kuuwa hapa nchini na mkoa wa Kilimanjaro pia nimekua nikishuhudia wagonjwa wenye saratani hiyo na bahati mbaya wanakuja kwenye hatua za mwisho hivyo kinga ni bora zaidi na imethibitika na WHO, TMDA na mashirika mengine ya kiusalama kuwa chanjo hii ni salama na haina madhara au matatizo ya ugumba kama baadhi ya wazazi wanavyodhani.
“Tangu Mwaka 2014 tulipoanza kuchanja kwa mkoa wa Kilimanjaro takwimu zinaonesha mabinti wengi walioanza kuchanja wakati huo ni wake za watu na wanawatoto kwa Sasa”, amesema afisa wa afya mkoa Kilamanjaro, Hapinus Pilalu.
No comments:
Post a Comment