MAELEZO YA MHESHIMIWA KASSIM MAJALIWA MAJALIWA (MB.), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUHITIMISHA HOJA YA BAJETI YA OFISI YA WAZIRI MKUU, TAASISI ZAKE NA MFUKO WA BUNGE KWA MWAKA 2024/2025 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, April 15, 2024

MAELEZO YA MHESHIMIWA KASSIM MAJALIWA MAJALIWA (MB.), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUHITIMISHA HOJA YA BAJETI YA OFISI YA WAZIRI MKUU, TAASISI ZAKE NA MFUKO WA BUNGE KWA MWAKA 2024/2025


UTANGULIZI
 
Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima na afya njema hata leo tumeweza kukutana kwenye Kikao hiki cha Sita cha Mkutano wa 15 wa Bunge la 12 kwa ajili ya kuhitimisha mjadala kuhusu Hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2024/2025.

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru na kukupongeza sana wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wote wa Bunge kwa uongozi wenu imara na thabiti. Sina shaka Waheshimiwa Wabunge wenzangu mtakubaliana nami kuwa wameongoza vema kipindi chote cha mjadala kuhusu hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2024/2025.

Mheshimiwa Spika, ninawashukuru na kuwapongeza sana Wenyeviti na Wajumbe wote wa Kamati za Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kwa michango yao muhimu. Nikiri kwamba maoni na ushauri wao wakati wote umekuwa ukileta tija kubwa kwenye Hoja ya Waziri Mkuu. 

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitowashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote kwa hoja na michango yenye tija katika kipindi chote cha mjadala wa Hoja ya Bajeti ya Waziri Mkuu. Niwahakikishie kwamba Serikali wakati wote itazingatia maoni na ushauri mnaoutoa katika mipango na utekelezaji wa majukumu yake kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wa Tanzania. 

Mheshimiwa Spika, kipekee ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Doto M. Biteko (Mb.) Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mawaziri wa Sekta na Naibu Mawaziri waliochangia Hoja ya Bajeti ya Waziri Mkuu.


Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia, kuwashukuru Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Idara, Mashirika, Taasisi na Wakala wa Serikali kwa ushirikiano mkubwa walioutoa na kufanikisha Hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, ninawapongeza sana Watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya katika hatua zote za maandalizi ya Hotuba ya Bajeti hadi tunapoelekea kuhitimisha mjadala wa Hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Vilevile, ninawashukuru kwa ushirikiano wanaonipatia ambao wakati wote umeniwezesha kutimiza majukumu yangu.

  SALAMU ZA POLE 

Mheshimiwa Spika, wakati tukiendelea na mkutano huu wa 15 wa Bunge lako tukufu, mnamo tarehe 9 Aprili, tuliondokewa na mpendwa wetu, Mheshimiwa Ahmed Yahya Abdulwakil, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kwahani. Sina shaka Waheshimiwa Wabunge wenzangu mtakubaliana nami kuwa Marehemu Ahmed Yahya Abdulwakil alikuwa na uwezo mkubwa na ushawishi wa kipekee ndani ya Bunge hili na mchango wake utakumbukwa daima.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kutoa salamu za pole kwa wana CCM wote, familia, ndugu na jamaa wa marehemu, wananchi wa jimbo la Kwahani na Watanzania wote kwa ujumla. Niwaombe Watanzania wote tumwombee marehemu kwa Mwenyezi Mungu apumzike mahali pema peponi. Amina.

 Mheshimiwa Spika, hivi karibuni wapo Watanzania wenzetu waliopatwa na majanga mbalimbali yakiwemo ajali za barabarani, mafuriko na mengineyo yaliyosababisha vifo na uharibifu wa mali. Kwa masikitiko makubwa ninaungana tena na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa salamu za pole kwa waathirika wote wa majanga hayo. Nitumie nafasi hii kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao kutokana na majanga hayo. Tumwombe Mwenyezi Mungu awajalie uponyaji wa haraka majeruhi wote na kuwapa pumziko la amani marehemu wote. Amina!


 WACHANGIAJI

Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala huu ukiendeshwa Waheshimiwa Wabunge 129 walichangia hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kati yao, Waheshimiwa Wabunge 119 walichangia kwa kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge 10 walichangia kwa maandishi. 

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia Hoja ya Waziri Mkuu. Ningependa kuwataja majina yao lakini kutokana na ufinyu wa muda, ninaomba uridhie nisiwataje na badala yake majina yao yaingizwe kwenye hansard. 

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wametoa ufafanuzi wa hoja nyingi zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge wakati tukiendelea na mjadala wa hoja ya Waziri Mkuu sikusudii kuzirudia. Nilihakikishie Bunge lako tukufu kuwa Waheshimiwa Mawaziri wataendelea kufafanua zaidi baadhi ya hoja zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge kwenye mjadala huu wakati wakiwasilisha hoja za bajeti za sekta zao. Kadhalika, kama ilivyo ada, Serikali itatoa ufafanuzi zaidi kuhusu hoja zilizosalia kwa maandishi. 

 MIAKA MITATU YA UONGOZI WA AWAMU YA SITA 

 Mheshimiwa Spika, kama Waheshimiwa Wabunge mnavyofahamu tayari tumetimiza miaka mitatu ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni jambo la kujivunia kuwa katika kipindi hicho cha miaka mitatu ya uongozi wake, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa taifa letu. Sisi sote ni mashahidi amekuwa kinara katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020. Mheshimiwa Rais wakati wote amekuwa akionesha busara, uhodari mkubwa, uzalendo, usikivu, uwajibikiaji na kuwa mfano wa kuigwa ndani na nje ya nchi.


 Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuungana na Watanzania wenzangu kumshukuru kwa uzalendo wake na namna anavyojitoa kulitumikia Taifa letu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali. Miradi hiyo inahusisha sekta za maji, elimu, afya na miundombinu ambayo niliieleza wakati nikiwasilisha hoja yangu. Ninaomba sasa nieleze kwa uchache mafanikio mengine yaliyopatikana.

KULETA MARIDHIANO YA KISIASA,AMANI NA UTULIVU WA KIDEMOKRASIA NCHINI

 Mheshimiwa Spika, sina shaka Waheshimiwa Wabunge wenzangu mtakubaliana nami kuwa Mheshimiwa Rais ni kinara katika kuimarisha demokrasia, haki za binadamu na utawala bora. Katika kipindi hiki cha uongozi wake, tumeshuhudia utekelezaji falsafa yake ya 4R (Reconciliation, Resilience, Reform and Rebuilding), kwa Lugha ya Kiswahili ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Mabadiliko ambayo kwa hakika imekuwa chachu ya kuimarisha siasa za ndani ya nchi yetu.

 Mheshimiwa Spika, kutokana na utashi wake mwelekeo wa mitazamo na uendeshaji wa masuala ya kisiasa umebadilika na kuchagiza siasa za kistaarabu. Sote ni mashuhuda kuwa nchi yetu inaendelea kuwa na mshikamano, amani na umoja wa Kitaifa. Hii ni kutokana na msisitizo wake kuhusu utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu, utawala bora na demokrasia.

 Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza masuala ya demokrasia kwa vitendo, tumeshuhudia maboresho mbalimbali ya upande wa mifumo, sheria na uendeshaji wa shughuli za kisiasa hapa nchini. Licha ya hayo, tumeshuhudia uwepo wa fursa zaidi za mijadala na maridhiano miongoni mwa makundi ya wadau wa demokrasia na masuala ya siasa hapa nchini. 


MABORESHO YA MFUMO WA UTOAJI HAKI NA TAASISI ZA HAKIJINAI


 Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha mfumo wa utoaji haki unaboreshwa, mnamo tarehe 31 Januari, 2023, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliunda Tume maalum, aliyoipa jukumu la kushauri namna njema ya kuboresha mfumo na utendaji kazi wa taasisi zinazohusika na haki jinai.

 Mheshimiwa Spika, Tume hiyo, ilipokea maoni kutoka kwa wananchi na wadau wengine wa hakijinai na kutoa mapendekezo ya maboresho yanayohitajika kufanyika. Tangu Tume ilipowasilisha mapendekezo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za maboresho ya mfumo wa utoaji wa hakijinai ikiwemo kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa Taasisi za Hakijinai. 
Mheshimiwa Spika, licha ya hayo, Serikali inaendelea kufanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa kwa lengo la kuhakikisha kuwa wananchi wanapata haki zao kwa wakati ili waweze kuendelea kufanya shughuli za maendeleo yao binafsi na Taifa zima kwa ujumla. Hii ndiyo dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kukidhi kiu na matarajio ya wananchi ya utoaji wa hakijinai kuanzia hatua za uchunguzi, ukamataji wa watuhumiwa hadi utoaji wa hukumu yenye haki mahakamani.

  Matumizi ya TEHAMA na Lugha ya Kiswahili Mahakamani

 Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kufanya jitihada kubwa kuimarisha matumizi ya TEHAMA ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia kutokana na mapinduzi ya nne ya viwanda duniani. Jitihada hizo zimeanza kuleta mafanikio katika utendaji wa Serikali kwa kuunganisha Serikali yote (Wizara, Idara, Wakala na Taasisi zake) ziweze kusomana kimfumo. Tumeanza kupata mafanikio Mfano: Mahakama ya Tanzania, ambapo mifumo mbalimbali ya TEHAMA imejengwa ili kurahisisha na kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi. 

 Mheshimiwa Spika, mifumo hiyo ni pamoja na Mfumo wa Usajili, Uendeshaji na Usimamizi wa Mashauri kwa ajili ya kurahisisha, kuharakisha na kuokoa muda wa mwenendo wa shauri Mahakamani. Mfumo mwingine ni wa unukuzi na kutafsiri mienendo ya mashauri Mahakamani kwa lengo la kuwa suluhu ya kudumu ili kuwawezesha Waheshimiwa Majaji na Mahakimu kuondokana na adha ya kuandika kwa mkono mwenendo wa mashauri. 

 Mheshimiwa Spika, hii ni hatua kubwa sana kwani mfumo huo unarekodi sauti na kupeleka kwenye maandishi. Vilevile, unaweza kutafsiri Lugha ya Kiswahili au Kiingereza kulingana na uhitaji. Kwa upande mwingine, Kanuni za Mahakama zimeanza kutafsiriwa sambamba na uandaaji wa mihtasari ya hukumu katika Lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi kuelewa mwenendo wa mashauri.

 Mafanikio Kwenye Sekta za Uzalishaji (Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Viwanda)

  Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuinua sekta ya uzalishaji. Kama mnavyofahamu, uzalishaji kupitia sekta ya kilimo umeendelea kuongezeka na kuiwezesha sekta hii kuchangia asilimia 26 ya pato la Taifa kwa mwaka. Jitihada zinazofanywa na Serikali ni katika kuhakikisha kuwa sekta ya kilimo inandeelea kutoa mchango mkubwa katika upatikanaji wa ajira, malighafi za viwandani, kuleta fedha za kigeni kutokana na mauzo nje ya nchi pamoja na kulihakikishia Taifa letu usalama wa chakula. Jitihada mbalimbali zinazofanywa zimewezesha nchi yetu kuwa na utoshelevu wa chakula kwa asilimia 124.

 Mheshimiwa Spika, sina shaka Waheshimiwa Wabunge mtakubaliana nami kuwa, Mheshimiwa Rais amefanya jitihada kubwa kuimarisha sekta ya uvuvi. Utekelezaji wa ujenzi wa mradi mkubwa wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko unaogharimu shilingi bilioni 289.5 ni kielelezo tosha cha dhamira njema ya Mheshimiwa Rais. Tayari ameshatoa ridhaa ya matumizi ya shilingi bilioni 106.2 za kuendeleza ujenzi wa bandari hiyo ambayo itachochea ukuaji wa sekta ya uvuvi na kuongeza pato la wananchi kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.

Kwa upande wa Sekta ya Mifugo, tumeshuhudia ikiendelea kuimarika na kuwezesha kutoa ajira kwa wananchi zaidi ya milioni 4.5. Aidha, kutokana na jitihada zilizopo mchango wa sekta katika Pato la Taifa umefikia asilimia 7.1 kwa mwaka. Uwekezaji kwenye viwanda umeongezeka ili kuzalisha bidhaa kwa mahitaji ya ndani na kupata masoko ya bidhaa zetu nje ili kuongeza pato la kigeni.

MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA 

 Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kupambana na tatizo la dawa zakulevya hapa nchini. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kundi la vijana ambao ni nguvukazi ya Taifa inayotarajiwa kuharakisha maendeleo ndiyo waathirika zaidi na matumizi ya dawa za kulevya nchini.
 
Mheshimiwa Spika, licha ya tatizo la dawa za kulevya kuendelea kuwepo hapa nchini, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya katika kipindi kifupi imefanya kazi kubwa. Tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua anazozichukua za kuiwezesha Mamlaka kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. 

Mheshimiwa Spika, Mamlaka inafanya kazi kubwa na nzuri, katika hili ninatoa rai kwa Taasisi za Serikali, Taasisi Binafsi, Mashirika ya Dini, Taasisi zisizo za Serikali na Washirika wa Maendeleo na wananchi wote kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa Mamlaka ili iweze kutimiza majukumu yake. Vilevile, ninawaomba kila mmoja kwa nafasi yake ashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Taasisi inaendelea kufanya kazi nzuri ya kudhibiti uzalishaji, usafirishaji, wauzaji na watumiaji.

Mheshimiwa Spika, ninawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango mliyoitoa kuhusu udhibiti na mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya. Umoja ni ushindi. Hivyo basi, Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wananchi wote tushirikiane katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Kwa pamoja tutashinda, mapambano yanaendelea.

UTEKELEZAJI WA SERA NA FURSA ZA KUJIKWAMUA KIUCHUMI

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza sera mbalimbali za uwezeshaji wa makundi maalum ya Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu. Lengo likiwa ni kuhakikisha makundi haya yanashiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi hapa nchini. 

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa sera hizo unafanywa kupitia mifuko ya uwezeshaji kiuchumi ambayo imeendelea kunufaisha makundi yote wakiwemo wanawake, vijana na wenye ulemavu. Katika mwaka 2023/2024, fedha kiasi cha shilingi bilioni 743.7 zimetolewa kwa wanufaika zaidi ya milioni sita kupitia Mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa Sera ya Ushirikishwaji wa Watanzania kwenye miradi ya kimkakati na uwekezaji nchini, wanawake na vijana wameendelea kunufaika kupitia miradi ya kimkakati na uwekezaji. Katika mwaka 2023/2024, jumla ya Watanzania 162,968 wamenufaika na ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. 

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuratibu masuala ya uzalishaji wa fursa za ajira nchini kwa kujenga mazingira wezeshi kwa wawekezaji na kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, fursa za ajira 2,489,136 zimezalishwa sawa na wastani wa ajira mpya 829,712 kwa mwaka. 

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwawezesha vijana ili waweze kujiari, kushiriki kwenye shughuli za maendeleo na kuchangia katika Pato la Taifa. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, kiasi cha shilingi bilioni 3.19 kimetolewa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambazo zilitumika kutoa mikopo kwa ajili ya kuwezesha miradi 148 katika sekta za kilimo, viwanda na biashara katika halmashauri 62. Aidha, Serikali imetoa mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi, kurasimisha na kuendeleza biashara kwa vijana katika maeneo mbalimbali nchini. Ofisi ya Rais - TAMISEMI hivi karibuni itatoa taarifa ya mfumo utakaotumika kutoa mikopo ya 10% kutoka Halmashauri nchini.

UTUNZAJI WA MAZINGIRA 

Mheshimiwa Spika, sote tunatambua kuwa uhifadhi wa mazingira una umuhimu mkubwa katika maisha yetu ya kila siku kwa kuwa unatuwezesha kupata mahitaji muhimu ikiwemo maji, chakula, madawa, malighafi za viwandani pamoja na nishati ya umeme itokanayo na maji. Ni ukweli usiopingika kuwa upatikanaji wa mahitaji haya unaharakisha maendeleo yetu ya kiuchumi na kijamii. Hivyo, tuna kila sababu ya kutunza mazingira ili nayo yaweze kututunza. 

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu huo, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa faida yetu na vizazi vijavyo. Vilevile, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara kwa mara amekuwa akitukumbusha kuhusu utunzaji wa mazingira yetu. Nami nitumie fursa hii kuungana na viongozi wetu kuzungumza kwa uchache kuhusu uhifadhi wa mazingira hapa nchini.

 Mheshimiwa Spika, kumekuwa na uharibifu mkubwa wa mazingira ambao kimsingi unasababishwa na ukataji miti ovyo kwa matumizi ya nishati; kilimo kisicho endelevu kinachofanyika kwa kukata miti na kuchoma mashamba ikiwa njia ya kurahisisha maandalizi ya shamba. Sababu nyingine ni ufugaji holela usiozingatia uwezo wa eneo la malisho ambao umesababisha mifugo kuharibu ardhi na maeneo yaliyohifadhiwa ikiwemo vyanzo vya maji.

 Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa athari za uharibifu wa mazingira ni mbaya kwa kuwa huathiri masuala ya kijamii na kiuchumi. Mathalan, mara kadhaa tumeshuhudia vifo vya mifugo kutokana na ukame na uhaba wa maji vilivyotokana na mabadiliko ya tabianchi yaliyosababishwa na uharibifu wa mazingira. Vilevile, mvua nyingi kupita kiasi zimeendelea kusababisha athari kubwa nchini ikiwemo mafuriko, vifo na uharibifu wa miundombinu mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa uhifadhi wa mazingira, nitumie fursa hii kusisitiza masuala yafuatayo:

Moja: Viongozi wote kuanzia ngazi ya vijiji hadi mikoa wasimamie kikamilifu uhifadhi wa mazingira na suala hili liwe ajenda ya kudumu katika vikao vyao;

Mbili: Viongozi wa Mikoa na Wilaya wasimamie utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu athari za kuchoma misitu ovyo, kufuga bila kuangalia uwezo wa maeneo ya kulishia, kufanya shughuli za kilimo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na kuondokana na tabia ya kukata miti ovyo;

Tatu: Halmashauri zote nchini zisimamie kikamilifu sheria ndogo za uhifadhi wa mazingira na kuwachukulia hatua watu wote wanaofanya uharibifu wa mazingira;

Nne: TFS na Halmashauri ziandae vitalu vya miti inayoendana na ikolojia ya maeneo yao, kuigawa kwa wananchi, kuhakikisha inapandwa na kukua. Hatua hii iende sambamba na kusimamia upandaji wa miti kwa kila kaya. Vilevile,TANROADS na TATURA wahakikishe wakandarasi wanapanda miti pembeni mwa kila mradi wa ujenzi wa barabara;

Tano: Wananchi waendelee kushirikiana na Serikali katika uhifadhi wa mazingira ili kuepusha madhara yatokanayo na uharibifu wa mazingira katika nchi yetu.

MABADILIKO YA HALI YA HEWA 

Mheshimiwa Spika, kasi ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani inaendelea kuongezeka kila mwaka na athari zake zimekuwa kubwa. Tathmini ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani imeonesha kuwa wastani wa ongezeko la joto kwa mwaka 2023 ulifikia nyuzijoto 1.4 kwa kipimo cha selsiasi, na kuvunja rekodi ya kuwa mwaka wenye joto kubwa zaidi katika historia ya dunia. Kwa upande wa Tanzania, wastani wa ongezeko la joto kwa mwaka 2023 ulifikia nyuzi joto 1.0 kwa kipimo cha selsiasi, na pia ulivunja rekodi kwa kuwa mwaka wenye joto kubwa zaidi katika historia ya nchi yetu. 

Mheshimiwa Spika, ongezeko la joto limesababisha uwepo wa El-Nino ambayo imeambatana na mvua kubwa na mafuriko. Hapa nchini, Oktoba hadi Desemba 2023 kulikuwa na ongezeko kubwa la mvua ambapo jumla ya milimita 534.5 zilipimwa ikilinganishwa na milimita 227.2 kwa mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia 135. Vilevile, ongezeko hilo la mvua kubwa limeshuhudiwa katika kipindi cha Januari hadi Aprili 2024. Kwa mujibu wa Taasisi ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua zitaendelea kunyesha hadi mwezi wa tano 2024 kwenye Mikoa ya Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi, Kusini na Nyanda za Juu Kusini.


USIMAMIZI NA UDHIBITI WA MAAFA

 Mheshimiwa Spika, kama ilivyo kwa nchi mbalimbali duniani nchi yetu imeendelea kupata mvua nyingi zaidi ya wastani kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababisha maafa mbalimbali. Maafa hayo ni pamoja na vifo, uharibifu wa mazao, makazi, mali za wananchi, miundombinu kama vile barabara, madaraja na reli. Kama mnavyofahamu, maeneo mengi yameathirika na mvua hizo ikiwemo, Mikoa ya Arusha, Lindi, Manyara, Kigoma, Morogoro, Pwani na Mbeya. Kamati ya Maafa ya Kitaifa kwa kushirikiana na Kamati za Mikoa na Wilaya imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kurejesha hali katika maeneo yaliyoathirika ikiwemo Wilaya za Rufiji (Muhoro), Kibiti (Delta), Newala, Lindi mjini, Liwale, Arusha (Kisongo), Malinyi, Kilombero, Mlimba (Masagati na Utengule), Mbeya (Kawetele). Hatua hizo ni pamoja na kutoa misaada ya kibinadamu kwa waathirika, kurejesha miundombinu iliyoathirika, kutoa elimu kwa jamii kuhusu kujikinga, kuchukua tahadhari na kuendelea kufanya tathmini ya kina ya athari na vyanzo vya maafa hayo. Kamati za Maafa ya Kitaifa inaendelea na kufanya tathmini maeneo yote.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuchukua hatua za haraka na dharura ikiwemo uokoaji, kutoa chakula, maji, makazi ya muda, dawa, mbegu na huduma za unasihi, katika maeneo yaliyopata athari kubwa za mvua zinazoendelea. Ninatoa pole kwa ndugu zetu walioathirika na mvua hizo na ninawaomba wananchi wote kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua kubwa zinazoendelea kunyesha hapa nchini. Ninawasihi sana wananchi kuwa na subira pindi wanapoona maji mengi yanapita hususan barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.

 Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa waendesha vyombo vya usafiri na wavuka kwa miguu kuchukua tahadhari ya kutovuka mahali panapo katiza maji juu ya barabara ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

Mheshimiwa Spika, TANROADS, TARURA na Shirika la Reli waendelee kuchukua hatua za haraka wakati uharibifu wa miundombinu ya barabara na reli unapojitokeza. Hatua hizo ziende sambamba na kutoa taarifa kwa watumiaji wa miundombinu hiyo, kuweka alama za tahadhari na kuweka kambi maalum za matengenezo katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

Mheshimiwa Spika, nizikumbushe Mamlaka za Upangaji kuzingatia mipango ya matumizi bora ya ardhi pamoja na kusimamia upangaji wa makazi kwa kuzingatia sheria ya Mipango Miji. Aidha, Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Sekta mtambuka waendelee na mikakati ya ujenzi wa miundombinu ya kuvuna maji ya mvua na kuyahifadhi kwa ajili ya huduma za jamii na uzalishaji ikiwemo kilimo na kupunguza athari za uharibifu wa mazingira.

 Mheshimiwa Spika, niwakumbushe watendaji wote wa Serikali kusimamia uratibu wa maafa kwa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022. na kanuni zilizopo. Aidha, Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa (2022) umeweka bayana majukumu ya kukabiliana na maafa kwa kuanzia ngazi za Kijiji au Mtaa, Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa kupitia Kamati za Usimamizi wa Maafa zilizopo katika ngazi husika. Hivyo basi ninasisitiza kuwa Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi zote ziendelee kuweka mipango madhubuti na kutekeleza majukumu ya usimamizi wa maafa katika ngazi husika pamoja na kutoa elimu ya kutoishi maeneo ya mabonde ili kuepusha kutokea maafa kama tunavyoshuhudia sasa baadhi ya maeneo.

DIRA MPYA YA TAIFA YA MAENDELEO 

 Mheshimiwa Spika, tarehe 03 Aprili, 2024 wakati nawasilisha Hotuba yangu ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2023/2024 na mwelekeo wa Kazi zake kwa Mwaka 2024/2025 nililieleza Bunge lako tukufu kuhusu mchakato wa maandalizi ya dira mpya ya maendeleo ya Taifa. Niruhusu niwapitishe Waheshimiwa Wabunge katika mafanikio yaliyopatikana katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 pamoja na maandalizi ya dira mpya ya Taifa ya maendeleo. 

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 umewezesha Taifa letu kuwa na mafanikio yafuatayo:

Moja: Kuboresha hali ya maisha ya Watanzania ikiwemo utoshelevu wa chakula; kuimarika kwa huduma za jamii hususani afya, elimu na upatikanaji wa maji; ongezeko la idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi na utawala katika maeneo mbalimbali nchini; kuongezeka kwa umri wa kuishi kwa Watanzania; na kupunguza kiwango cha umaskini wa kutupwa.

Mbili: Kuimarika kwa mazingira ya amani, usalama na umoja ikiwemo kuzingatiwa kwa utii wa sheria na utawala wa kisheria kulikowezesha kupungua kwa matukio ya uhalifu wa aina mbalimbali hususan mauaji, wizi wa watoto, unyanganyi wa kutumia silaha; wizi katika barabara kuu, uhalifu wa kifedha na dawa za kulevya.

Tatu: Kuimarika kwa utawala bora ikiwemo utaratibu wa makabidhiano ya kiuongozi na kiutawala kwa amani na utulivu; kuongezeka kwa kiwango cha haki za msingi za binadamu; na kuendelea kupungua kwa kiwango cha rushwa nchini. 

Nne: Kuwepo jamii iliyoelimika vema na inayojifunza ambapo idadi ya Watanzania wanaopata elimu rasmi imeongezeka katika ngazi mbalimbali (ngazi ya elimu ya msingi, sekondari na vyuo vikuu). Aidha, kumekuwa na ongezeko kubwa la nyenzo na fursa za kuwezesha kuendelea kujifunza kupitia uwepo wa majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Tano: Uchumi kuimarika na kuweza kukabiliana na ushindani kutoka nchi nyingine kulikochangia kuongezeka kwa mchango wa pamoja wa sekta ya viwanda, ujenzi na uzalishaji kwenye Pato la Taifa; kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi kupitia sekta ndogo ya uzalishaji; kuhimili kiwango cha mfumuko wa bei kwa chini ya tarakimu moja; ongezeko la Pato la Taifa kwa mwaka kwa wastani wa asilimia 6.7 kati ya mwaka 2000 na 2021; kuimarika kwa miundombinu ya msingi na ya kiuchumi hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, huduma za mawasiliano, na huduma za umeme.

Matarajio ya Dira Mpya ya Taifa

Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana yanatokana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambayo itafikia tamati ifikapo Juni, 2026. Sasa tupo kwenye mchakato wa maandalizi wa dira mpya ya Taifa ya maendeleo inayotarajiwa kuanza mwaka 2026/2027. Ni matarajio yetu kuwa utekelezaji wa Dira mpya utawezesha nchi yetu kupiga hatua zaidi kimaendeleo. 

Mheshimiwa Spika, dira mpya, pamoja na mambo mengine itazingatia masuala muhimu yafuatayo: kufungamanisha ukuaji wa uchumi na sekta za uzalishaji; kuimarisha upatikanaji wa data kwa sekta isiyo rasmi ili kuweza kurasimisha shughuli na kutambua mchango wake katika ukuaji wa uchumi; kuboresha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini; kuwepo na uratibu jumuishi wa programu mbalimbali za utekelezaji wa dira mpya; kutoa kipaumbele katika ufanisi wa mashirika ya umma wakati wa utekelezaji wa dira mpya; kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi ndani na nje ya nchi pamoja na kuwawezesha wenyeji kuwa na utayari wa kupokea na kushirikiana na wageni wanaokuja kuwekeza na kufanya biashara nchini; kuweka mkazo zaidi katika suala la maadili ya Taifa; na kubainisha mapema viashiria hatarishi na namna ya kukabiliana navyo.

 Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine nitumie fursa hii kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maandalizi wa dira yetu mpya.

MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA MUUNGANO 

 Mheshimiwa Spika, wakati tunaelekea kutimiza miaka 60 ya muungano wetu sote ni mashahidi kwamba, muungano wa Tanganyika na Zanzibar umedumu na umekuwa wa kipekee na wa kuigwa Barani Afrika na Duniani kwa ujumla. Vilevile, sote tunatambua kwamba jitihada kubwa zimefanyika katika kulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni Tunu ya Taifa letu. Matunda ya muungano wetu yanajumuisha kuimarika kwa utaifa, umoja, amani, utulivu na hali ya maisha ya wananchi kutokana na ukuaji wa uchumi wa pande zote mbili za Muungano. 

 Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuutunza muungano wetu ulioasisiwa na kuenziwa kwa manufaa ya Watanzania kwa kizazi cha sasa na baadae Serikali ilizindua kitabu kinachoelezea historia, chimbuko, misingi na maendeleo ya muungano. Vilevile, elimu kwa umma kuhusu muungano imekuwa ikitolewa kupitia vipindi vya redio na televisheni, magazetini, semina, warsha, makongamano, maonesho ya kitaifa, ziara za viongozi, machapisho mbalimbali na mitandao ya kijamii.

Mheshimiwa Spika, ninayo furaha kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa tarehe 26 Aprili, 2024 nchi yetu itaadhimisha miaka 60 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Maadhimisho hayo yataongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

 Mheshimiwa Spika, matukio yaliyopangwa kufanyika ni pamoja na Uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Muungano yaliofanyika Zanzibar tarehe 14 Aprili, 2024. Matukio mengine ni Uzinduzi wa Maonesho ya Muungano yatakayofanyika tarehe 19 Aprili, 2024 katika Viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam; na Dua na Sala ya kuliombea Taifa tarehe 22 Aprili, 2024 katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma. Nitumie fursa hii kuwajulisha Watanzania kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na wote wanaalikwa kushiriki katika matukio hayo muhimu.

 Mheshimiwa Spika, matukio haya ni muhimu katika kuimarisha muungano wetu ikiwa ni njia moja wapo ya kuwaenzi waasisi wa muungano wetu, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuwapa pumziko la amani waasisi wa muungano wetu. 

UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

 Mheshimiwa Spika, kama Waheshimiwa Wabunge mnavyofahamu, Taifa letu mwaka huu litakuwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Uchaguzi huo ni muhimu sana kutokana na ukweli kwamba Viongozi wa Serikali za Mitaa ni msingi imara katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Taifa letu. 

Mheshimiwa Spika, licha ya hayo, Viongozi wa Serikali za Mitaa ni wasimamizi wa karibu wa shughuli za maendeleo ya wananchi lakini pia wanalo jukumu kubwa na kuhakikisha ulinzi na usalama wa wananchi katika maeneo yao. Kutokana na umuhimu huo ninapenda kusisitiza kuhusu masuala yafuatayo:

Moja: Watanzania wenzangu bila kujali jinsia watumie haki yao ya Kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa. Wale wenye uwezo jitokezeni kugombea nafasi za uongozi pamoja na kushiriki kikamilifu siku ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Watanzania wote wajitokeze kwa wingi ili kushiriki katika hatua zote za uchaguzi huo ikiwemo maboresho ya daftari la mpigakura; 

Pili: Viongozi wa Serikali tumieni kila fursa zikiwemo semina, warsha na mikutano kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika uchaguzi huo. Wekeni mkakati wa kutoa elimu kwa umma ili ufahamu kuhusu haki na wajibu wao katika kuwachagua viongozi; na

Tatu: Wamiliki wa vyombo vya habari wekeni mkakati wa kuhamasisha umma wa Watanzania kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Andaeni makala maalum na vipindi kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi.

Kutambua Mchango wa Watumishi wa Umma

Mheshimiwa Spika, watumishi wa umma wana mchango mkubwa katika kutafsiri na kutekeleza maono ya Mheshimiwa Rais. Mafanikio tunayoyashuhudia katika utekelezaji wa mikakati ya maendeleo ya Taifa ni kutokana na kazi nzuri inayofanywa na watumishi wa umma. Nitumie fursa hii kuwapongeza kwa dhati watumishi wote kwa kujitoa na kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.
  
Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo niwakumbushe watumishi wenzangu kuimarisha ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi na kutekeleza kikamilifu wajibu tulionao. Watumishi wote tujikite katika kutatua changamoto na kero za wananchi, tuwafuate kwenye maeneo yao, tuwasikilize na kutoa majawabu yanayohitajika. Kwa kufanya hivyo wananchi wataishi kwa amani na utulivu na kuendeleza shughuli za uzalishaji mali. 

UFAFANUZI WA HOJA

WATOA HOJA: Mheshimiwa Kasalali Emanuel Mageni (Mbunge wa Jimbo la Sumve), Mheshimiwa Ester Amos Bulaya (Viti Maalum) na Mhe. Janejelly Ntate James (Viti Maalum)
HOJA: Serikali kufanya marekebisho ya ulipaji wa mafao ya wafanyakazi kupitia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Serikali iongeze wigo wa utoaji wa elimu ya Kanuni mpya ya mafao kwa watumishi kwa lengo la kujenga uelewa.

MAJIBU YA HOJA

Kanuni mpya ya ulipaji wa mafao ilianza kutumika tarehe 1 Julai 2022 kwa kuzingatia tathmini ya uhimilivu na uendelevu wa Mifuko iliyofanyika katika kipindi husika. Serikali imesikia na kupokea maoni mbalimbali ya wadau wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, wafanyakazi na vyama vya waajiri na wafanyakazi. Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha mafao kwa wastaafu na itaendelea kufanya tathimini kwa kuzingatia sheria za kazi. Aidha, kuhusu utoaji elimu ya kanuni ya mafao kwa watumishi; Serikali itaendelea kutoa elimu ya hifadhi ya jamii ikiwemo mafao kwa watumishi kupitia njia mbalimbali. Nitumie fursa hii kumtaka Waziri wa Kazi na Ajira asimamie kuongeza wigo wa utoaji wa elimu ya mafao kwa watumishi kwa lengo la kujenga uelewa wa kutosha. 

MTOA HOJA: Mheshimiwa Ahmed M. Shabiby (Mbunge wa Jimbo la Gairo)
HOJA: Serikali ihakikishe inaweka mikakati ya kuwezesha upatikanaji wa vyanzo vingi vya mapato ili kuwezesha upatikanaji wa bima za afya kwa wananchi wa vijijini.

MAJIBU YA HOJA
Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya Mwaka 2023 imeanzisha Mfuko kwa ajili ya kugharimia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo na kubainisha vyanzo vya fedha vya Mfuko huo. Serikali itaendelea kupokea mapendekezo ya uendeshaji wa mfuko ikiwemo vyanzo vya mapato na kufanya maboresho kadri inavyofaa.

 MTOA HOJA: Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko (Viti Maalum)
HOJA: Wanyamapori kuvamia maeneo ya wananchi na mauaji ya watu kwenye hifadhi.

MAJIBU YA HOJA

Serikali inatambua uwepo wa changamoto ya baadhi ya wanyamapori kuvamia makazi na mashamba na kusababisha madhara kwa wananchi waishio karibu na hifadhi. Madhara hayo ni pamoja na ulemavu, vifo na uharibifu wa mali. Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu kukabiliana na wanyama waharibifu, uanzishaji wa vituo vya ulinzi kwa maafisa wanyamapori.

Kwa upande mwingine kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi na kusababisha migogoro baina yao na askari wa hifadhi ambayo imekuwa ikisababisha majeruhi au vifo vya wananchi na askari wa hifadhi. Nitumie fursa hii kuwakumbusha wasimamizi wa hifadhi kuzingatia taratibu wakati wa kushughulikia changamoto za uvamizi hifadhini. Kwa upande mwingine niwasihi wananchi kuheshimu mipaka ya maeneo yaliyohifadhiwa na kuacha tabia ya kuingia hifadhini kiholela, kuingiza mifugo, kufanya shughuli za kilimo ndani ya hifadhi na uwindaji haramu.

 MTOA HOJA: Mheshimiwa Kasalali Emanuel Mageni (Mbunge wa Jimbo la Sumve), 

HOJA: Utekelezaji wa Ahadi za Mawaziri

MAJIBU YA HOJA: 

Serikali inaendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020-2025 na ahadi za viongozi katika maeneo mbalimbali kupitia mipango na bajeti ya kila mwaka. Utekelezaji unaofanyika utaendelea mpaka mwezi Juni, 2025.

  HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, wakati tunaelekea kuhitimisha hoja hii ya Waziri Mkuu, naomba nitumie nafasi hii kuzungumzia masuala yafuatavyo:

Mafanikio ya Sekta ya Michezo
Mheshimiwa Spika, sote ni mashahidi katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, sekta ya michezo imepata mafanikio makubwa. Michezo inapendwa na Watanzania walio wengi na imekuwa chachu ya maendeleo na nguzo muhimu kwa ustawi wa jamii pamoja na kuitangaza nchi yetu kimataifa na kuliletea sifa Taifa.

Mheshimiwa Spika, mtakubaliana nami Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mpenda michezo na amekuwa mstari wa mbele kusimamia ukuaji wa sekta ya michezo. Maono na maelekezo yake yameleta mchango mkubwa na mafanikio katika sekta hii. Aidha, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa kinara katika kuongeza hamasa kwa wanamichezo wetu, suala ambalo limechangia na kuimarika kwa nafasi ya Taifa kwenye michezo mbalimbali ya Kimataifa hususan ngumi, riadha na mpira wa miguu.

 Mheshimiwa Spika, kipekee nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa hamasa kubwa anayotoa katika sekta ya michezo pamoja na kuhamasisha wadau mbalimbali kuchangia timu zetu ili ziweze kufanya vizuri. Kama mtakumbuka kupitia Goli la Mama mafanikio makubwa yalipatikana katika michezo wa mpira wa miguu katika hili mama ameupiga mwingi na apewe maua yake!

Mheshimiwa Spika, vilevile, jitihada za Mheshimiwa Rais zimewezesha vilabu vyetu vya mpira wa miguu kuendelea kungara Kimataifa. Katika msimu wa 2023/2024 Tanzania imekuwa nchi pekee iliyoingiza timu mbili kwenye hatua ya robo fainali ya Mashindano ya Klabu Bingwa Afrika. Hatua hii ni ya kupongezwa na kujivunia kama taifa. Hongereni Sana!

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuvipongeza vilabu vyetu ya Simba na Yanga kwa kufikia hatua ya robo fainali. Ninawapongeza sana kwa kucheza mpira kwa viwango vya hali ya juu. Michuano yote ilikuwa mikali na kwa yeyote anayeufahamu mchezo wa mpira wa miguu atakubaliana nami kwamba wachezaji wetu walionesha mpira wa viwango vikubwa na kukonga mioyo ya washabiki wetu. 

Mheshimiwa Spika, nirudie kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu ama kwa hakika mmelitendea haki jukumu la kuishauri Serikali, la uwakilishi wa wananchi pamoja na kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 inatekelezwa kama ilivyoelekezwa. 
 
 Mheshimiwa Spika, nitumie pia fursa hii kutoa rai kwa Watanzania wote kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali yake. Dhamira ya Mama Samia ni safi ambayo ni kuwaletea maendeleo ya haraka Watanzania wote. Jitihada kubwa anaendelea kuzifanya, hivyo basi Watanzania wote tumpe ushirikiano unaohitajika ili aweze kufanikisha utekelezaji wa maono, mipango na mikakati ya kuinua ustawi wa Watanzania.

 Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa, naomba Bunge lako tukufu liridhie na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zilizo chini yake na Mfuko wa Bunge kama nilivyowasilisha katika hoja yangu ya tarehe 3 Aprili 2024. 

 Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa hoja.

No comments:

Post a Comment