NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Dkt Festo Dugange amesema katika mwaka wa fedha 2025/26 Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa itatenga Sh Milioni 100 kwa ajili ya kuongeza majengo na kuanza utaratibu wa kupandisha hadhi zahanati ya Madope kuwa kituo cha afya.
Mhe Dkt Dugange ametoa kauli hiyo leo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Ludewa, Mhe Joseph Kamonga aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kupandisha hadhi Zahanati za Madope na Ludewa kuwa vituo vya afya.
“ Zahanati za Madope na Ludende ni Zahanati zilizopo kwenye Makao Makuu ya Kata za Madope na Ludende Mtawalia. Zahanati ya Madope ina eneo la takribani ekari 10 pamoja na vigezo vingine inakidhi kuwa na kituo cha afya.
Katika mwaka wa fedha 2025/26 serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo itatenga Sh Milioni 100 kwa ajili ya kuongeza majengo na kuanza utaratibu wa kuipandisha hadhi kuwa kitio cha afya,” Amesema Mhe Dkt Dugange.
Kuhusu Zahanati ya Ludende amesema haikidhi vigezo vya kuwa kituo cha afya kwa kuwa ina eneo dogo (ekari 5), uchache wa watu na inapakana na kituo cha afya Mlangali.
No comments:
Post a Comment