Na Andrew Chale,Dar es salaam.l
USIKU wa tukio la Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu msimu wa pili , zilizofanyika usiku wa April 13, 2024, katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki, zimefana huku watu mbalimbali wakizipongeza.
Katika tukio hilo, burudani na matukio mbalimbali yaliweza kunogesha tuzo hizo ambapo mgeni wake rasmi alikuwa ni mshindi wa Tuzo ya Nobel wa mwaka 2021 kwa upande wa fasihi, Prof .Abdulrazak Gurnah.
Katika tukio hilo, Jumla ya washindi 30 walitangazwa wakati wa hafla hiyo iliyohudhuriwa na mamia ya watu, wakiwemo maafisa waandamizi wa Serikali, mabalozi, na wale wanaotoka kwenye tasnia ya uandishi nchini, kumi wakiwa ni waandishi bunifu kwenye tanzu ya riwaya, kumi wengine wakiwa ni washairi na kumi wengine wakiwa ni waandishi wa hadithi za watoto, ingizo jipya kwenye tuzo hizo.
Hafla hiyo ilianza kwa wahudhuriaji wake kutangaziwa washindi wa kumi mpaka wa saba kutoka kwa kili tanzu, ambao wote walitambuliwa kwa kupewa vyeti vilivyotambua ushiriki wao.
Hili lilifuatiwa na kuwekwa hadharani majina ya washindi wa tatu na wa pili kutoka kwa kila tanzu, ambao walijishindia vyeti na fedha taslimu Shilingi milioni tano kwa washindi wa tatu na Shilingi milioni saba kwa washindi wa pili.
Furaha ziliibuka wakati wa kutangazwa kwa washindi wa kwanza, Laura Pettie Kisswaka (riwaya), Blandina Isabela Lucas (hadithi za watoto) na Mohamed Omar Juma (ushairi) – ambao walizawadiwa vyeti, ngao na fedha taslimu Shilingi milioni kumi.
Mbali na zawadi hizo, washindi hao wa kwanza pia watashuhudia Serikali ikigharamia uchapishwaji wa miswaada yao na vitabu vitakavyotokana na miswaada hiyo vitasambazwa kwenye shule na maktaba zote zinazomilikiwa na Serikali nchi nzima.
Serikali hutafuta mchapishaji kwa utaratibu wa kutangaza zabuni ambapo wachapishaji wanaokizi vigezo huomba na kuchaguliwa.
Tuzo zinaandaliwa na Wizara ya Elimu huku zikisimamiwa na Taasi ya Elimu Tanzania (TET).
Uandishi bunifu ni aina ya uandishi ambapo mwandishi hubuni dunia yake katika kuelezea mawazo yake kuhusiana na mambo yanayoendelea katika jamii yake.
Aina hii ya uandishi huonekana kwenye kazi kama vile riwaya, ushairi na tamthiliya ambazo uandishi wake hutofautiana na ule unaohusu matukio ambayo yapo kwenye uhalisia wa kidunia.
Awali akitoa hotuba yake, Mgeni rasmi, Prof Gurnah amesema uandishi bunifu una umuhimu sana kwa taifa na dunia kwa ujumla kwani hutumika katika kuhifadhi historia, uchumi, siasa na utamaduni wa watu wenyewe, ambayo yote husaidia kujenga jamii thabiti kimitazamo na kitabia.
“Vilevile, maandiko bunifu huelimisha, huburudisha, na kuliwaza kulingana na nyakati tofauti ambazo jamii inapitia,” alihutubia Gurnah ambaye moja ya kazi zake bunifu, riwaya ya Paradise, imetafsiriwa kwa Kiswahili na Ida Hadjivayanis na kuitwa Peponi.
“Maandishi bunifu pia ni kichocheo cha kuchokonoa fikra yakinifu za watu kuhusu hali ya jamii.”
Prof Gurnah pia ameeleza kwamba, jamii zote ulimwenguni kote huchagizwa kwa maandiko yaliyoandikwa kwa lugha ya jamii husika, akitambua juhudi zinazotekelezwa na Serikali katika kukuza, kuendeleza na kuhifadhi maandiko bunifu ya Tanzania, hali aliyosema inasaidia “kufumbata” uhai wa taifa hilo la Afrika Mashariki.
“Natoa raia kwa waandishi wenzangu kutumia kalamu zetu ili kulifaa taifa letu la Tanzania,” Gurnah, ambaye kazi zake nyingi zinahusu madhila ya ukoloni na hatma ya wakimbizi wa Afrika barani Ulaya, aliwaasa waandishi wenzake. “Waswahili husema, kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza.
Waandishi wenzangu, ikumbukwe kuwa uvumilivu na ustahimilivu wenye kuchochewa na kupenda kujifunza ndiyo msingi wa mafanikio katika tasnia ya uandishi bunifu.”
Gurnah alizungumza kuhusu kukua kwa lugha ya Kiswahili duniani, akisema lugha hiyo imekuwa “tunu” barani Afrika na “mwezi mchanga unaochomoza mataifani na viungani mwao,” hali inayoweka ulazima wa upatikanaji wa machapisho mengi zaidi yaliyopo kwenye Kiswahili, hali itakayoitambulisha lugha hiyo na kuipaisha zaidi.
Mwandishi Nyerere
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alielezea mantiki ya tuzo hizo kupewa jina la Mwalimu Nyerere, akisema hatua hiyo imefanyika kumuheshimisha kiongozi huyo wa kwanza wa Tanzania huru anayejulikana kwa kupenda kwake sana kusoma na kuandika.
“Kweli, Mwalimu [Nyerere] alikuwa na mahaba na vitabu,” Profesa Mkenda, ambaye pia ni Mbunge wa Rombo (Chama cha Mapinduzi – CCM), alisema. “Alivisoma na alivichambua, na zaidi, alivitafsiri na aliviandika. Tunajua pia alitafsiri pia kitabu cha [mwanafalsa wa Kigiriki] Plato, ambacho tunatumaini tutakiona, tutazungumza na familia yake.”
“Leo [Aprili 13] tunaadhimisha kuzaliwa kwa Mwalimu Nyerere na tunamuenzi kwa kutoa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu,” aliongeza Mkenda.
“Hii ni tuzo kubwa sana inayozingatia umahiri na umaarufu wa Mwalimu Nyerere.”
No comments:
Post a Comment