WAZIRI MKUU AFUNGA MAONESHO YA WIKI YA NISHATI 2024 - OKULY BLOG

Breaking

Home Top Ad

TANGAZA NASI HAPA | PIGA 0785 364 965

Friday, April 19, 2024

WAZIRI MKUU AFUNGA MAONESHO YA WIKI YA NISHATI 2024

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akipata maelezo kuhusu Nishati Safi
ya Kupikia kutoka kwa Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na
Nishati Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi
Advera Mwijage wakati wa Maonesho ya Wiki ya Nishati Jijini Dodoma,
tarehe 19 Aprili 2024.
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa Maonesho ya
Wiki ya Nishati Jijini Dodoma, tarehe 19 Aprili 2024.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
akizungumza wakati wa Maonesho ya Wiki ya Nishati Jijini Dodoma,
tarehe 19 Aprili 2024.

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amefunga Maonesho ya Wiki ya Nishati katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma kutoa maagizo kwa
Wizara ya Nishati na Taasisi zake kuendelea kuboresha maonesho hayo na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mhe. Majaliwa ameitaka Wizara ya Nishati kuweka mkakati wa kuhakikisha maonesho hayo yanakuwa endelevu ili wabunge wapate fursa za
kuwasilisha hoja zao moja kwa moja kwa wataalam na kupewa majawabu ya hoja na changamoto zinazowakabili wao na wananchi wanaowakilishwa.

Aidha, ameagiza Maonesho ya Nishati yafanyike kuanzia ngazi ya wilaya, mikoa na halmashauri ili yale yanayofanyika Makao Makuu yabaki kuwa ya
Kitaifa.

Amefafanua kuwa kwa kufanya hivyo huduma zitakuwa zimesogezwa zaidi
kwa kwa wananchi na pia Mameneja wa TANESCO wa Kanda, Mikoa na Wilaya watoe ufafanuzi wa hoja na changamoto zinazowakabili wananchi husika.

Vilevile ameitaka Wizara kuweka mkakati wa kuwawezesha wananchi wote kupata ufafanuzi na fursa zinazotokana na miradi inayotekelezwa katika
Sekta ya Nishati.

Pia ameagiza maonesho hayo yafanyike maeneo yanayofikika kwa urahisi kwa wananchi wengi kama vile katikati ya miji ili wananchi wengi
washiriki na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali.

Vilevile Waziri Mkuu ameitaka Wizara isimamie na kuondoa mlundikano
wa maombi ya kuunganisha umeme kwa wananchi na TANESCO ihakikishe inaimarisha mfumo wa kupokea maombi na kutekeleza maombi hayo kwa
haraka.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa agizo kuwa Taasisi zote
zinazolisha watu wengi kuanzia 50 hadi 100 waanze kubadilisha
teknolojia ya kupikia na kutumia Nishati Safi ya Kupikia na ifikapo
mwisho wa mwaka 2024 Serikali inataka kuona asilimia 99 ya Taasisi za aina hiyo zinatumia Nishati Safi ya Kupikia.

Vilevile amempongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa
utendaji kazi wake ambao umechochea hali ya upatikanaji umeme nchini kuongezeka na kutosheleza mahitaji na pia kuwezesha upatikanaji wa
umeme wa ziada.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuendelea
kuboresha utoaji huduma ya umeme nchini.

Amesema, “ tunafanyakazi kubwa kubadilisha taswira ya Wizara ya
Nishati na Taasisi zake na niwashukuru sana watendaji wa Wizara hii na Taasisi zake kwa kufanyakazi kwa juhudi na niwaombe waongeze kasi.”
Amesema Dkt. Biteko.

Amewapongeza wakandarasi wa umeme kwa kuendelea na utekelezaji wa miradi ya nishati katika maeneo mbalimbali nchini, sambamba na kuvipongeza vyombo vya habari nchini kwa kuendelea kutangaza habari
zinazohusu masuala ya nishati kwa lengo la kujibu hoja na maswali
mbalimbali ya wananchi.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amesema kuwa sekta ya nishati ni moja kati ya sekta mtambuka nchini inayochagiza
maendeleo ya Sekta nyingine na kwamba ili maendeleo yapatikane sekta ya nishati ina mchango mkubwa.

Ameeleza mchango sekta ya umeme hauepukiki katika ngazi zote kuanzia
vitongoji hadi Taifa huku sekra ya uzalishaji ikiwemo viwanda na
migodi na maeneo mbalimbali huku akisisitiza kuwa umeme usitumike kwa ajili ya mahitaji ya awali pekee kama kuwasha taa na kuchaji simu.

Akizungumzia mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP)
amesema, “Bwawa la Julius Nyerere licha ya kuzalisha umeme litasaidia
masuala mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa maji hasa mikoa ya karibu na bwawa hivyo badala ya maji kupita tu kwenye mkondo wa maji basi
yahifadhiwe kwa ajili ya kusambaza kwa wananchi”. Amesema Mhe. Tulia.

Aidha, Mhe. Spika ameishauri Serikali kuanzisha gridi ya maji kama
ilivyo gridi ya umeme ambayo ipo katika maeneo mengi nchini ili
kusaidia usambazaji wa maji katika maeneo kame kwa kutumia gridi ya
maji.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. David Mathayo ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kuandaa maonesho ya Wiki ya Nishati ambayo yametoa fursa kwa Waheshimiwa Wabunge na
wananchi kupata uelewa kuhusu utekelezaji wa kazi zinazofanywa na
Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zake na kushauri maonesho hayo
kuwa endelevu.

Amesema Kamati yake itaendelea kushauriana na Wizara katika masuala mbalimbali yanayohusu nishati ikiwemo upelekeji wa huduma kwa wananchi wanaozunguka miradi mbalimbali hasa ya Gesi Asilia ili maisha yao
yaendane na thamani ya miradi hiyo.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba
alisema kuwa Wiki ya Nishati kwa mwaka 2024 imekuwa na mafanikio
makubwa kutokana na kuhudumia idadi kubwa ya Waheshimiwa Wabunge na wageni mbalimbali.

“Wabunge 267 wametembelea mabanda ya maonesho na kujionea kazi zinazofanywa na Wizara na Taasisi zake, kuuliza maswali na kutoa
maoni na wananchi 213 walitembelea maonesho haya” amesema Mhandisi
Mramba.

No comments:

Post a Comment

HABARI KUU KWA SASA

KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA KASI YA UJENZI KITUO CHA KUPOZA UMEME CHALINZE

Na Mwandishi wetu, Pwani. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeeleza kuridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wa mradi wa kituo cha...