Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Manyara imeendelea kufanya matengenezo ya miundombinu ya daraja la Losinyai lililopo katika eneo la kijiji cha Kastam Wilayani Simanjiro Mkoani wa Manyara.
Akizungumza na Kipindi cha TANROADS Mkoa kwa Mkoa tarehe 12 April 2024; Meneja wa TANROADS Mkoa wa Manyara Mha. Dutu J. Masele amesema matengenezo hayo yanafanyika katika daraja hilo linalounganisha Wilaya ya Simanjiro na Mkoa wa Arusha baada ya kuharibiwa na mafuriko ya maji ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha sehemu mbalimbali Nchini.
Amesema TANROADS kwa kutambua umuhimu wa daraja hilo wanafanya maboresho na matengenezo ya haraka ili kurejesha mawasiliano ya barabara lilipo daraja hilo na kuweza kuruhusu shughuli za kijamii kuendelea katika eneo hilo.
Mha. Masele amesisitiza kuwa timu ya Wahandisi kutoka Ofisi ya TANROADS Mkoa wa Manyara tayari imewasili katika eneo lililopata changamoto huku wakifanya kazi kwa nguvu zote kuhakikisha daraja hilo linaendelea kupitika.
No comments:
Post a Comment