BARAZA LA MAWAZIRI LAWAAMURU WAKENYA WANAOISHI KATIKA MAENEO YANAYOKUMBWA NA MAFURIKO KUHAMA NDANI YA SAA 48. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, May 1, 2024

BARAZA LA MAWAZIRI LAWAAMURU WAKENYA WANAOISHI KATIKA MAENEO YANAYOKUMBWA NA MAFURIKO KUHAMA NDANI YA SAA 48.


Rais wa Kenya William Ruto ametangaza kwamba raia wanaoishi katika maeneo yaliyo katika hatari ya mafuriko au maporomoko ya ardhi kote nchini watatakiwa kuhama kuanzia Jumatano. 


Bw Ruto alikuwa akizungumza katika eneo la Mai Mahiu, kaskazini mwa Nairobi ambapo wimbi la maji kutoka kwenye bwawa lililofurika lilisomba nyumba na watu Jumapili usiku. 


Rais alisema serikali imepanga maeneo yote tete ambayo yanaweza kukabiliwa na hatari hizo na lazima watu waanze kuhama mara moja kwa sababu kuna utabiri wa mvua kuendelea kunyesha. 


Huu sio "wakati wa kukisia," alisema, "uwezekano wa mafuriko na watu kupoteza maisha ni kweli."


Ruto Jumanne asubuhi aliitisha kikao Maalum cha Baraza la Mawaziri kujadili hatua za ziada zinazohitajika ili kupunguza athari za mvua zinazoendelea kunyesha na kusababisha maafa na kuharibu mali nchini humo.


Baraza la Mawaziri lilipokea na kuzingatia ripoti ya utabiri wa hali ya hewa kutoka Idara ya Hali ya Hewa, ikionyesha kwamba mvua zinazoendelea kunyesha zitazidi kunyesha kwa muda mrefu, na kuonya kwamba hali inaweza kuwa mbayakatika siku zijazo.


Liliagiza kwamba wananchi wanaoishi ndani ya maeneo haya hatari wanatakiwa kuhama ndani ya saa 48.


Haya ni pamoja na maeneo karibu na mabwawa na hifadhi nyingine za maji katika ardhi ya umma au ya kibinafsi, maeneo yanayokumbwa na maporomoko ya matope na maporomoko ya ardhi na maeneo ya kando ya mito na njia nyingine za maji nchini kote.


Wananchi wote walioathiriwa na agizo hili wataarifiwa kufikia mwisho wa siku ya Jumatano, Mei 1, 2024.


Serikali imeweka mikakati ya kuwasaidia watu kuhama maeneo hayo hadi kwenda makazi ya muda kwa wale ambao wataathiriwa na agizo hili endapo watahitaji msaada.


Wakati serikali ikihimiza watu kuhamakwa hiari, wale wote watakaobaki ndani ya maeneo yaliyoathiriwa na agizo hilo watahamishwa kwa nguvu kwa ajili ya usalama wao.


Mafuriko nchini Kenya yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 170 hadi sasa huku wengine maelfu wakiachwa bila makaazi na mkasa wa hivi punde katika eneo la Mai Mahiu ukisababisha vifo vya zaidi ya watu 50. 


Shughuli ya uokoaji inaendelea katika eneo hilo yapata kilomita 60 kutoka mji mkuu, Nairobi.

No comments:

Post a Comment