Nairobi, Mei 28, 2024 – Katika jitihada za kuboresha maisha na kukuza uchumi wa masoko inayoyahudumia, Benki ya CRDB imeendesha mjadala uliolenga kujadili ukuzaji wa huduma za benki zinazovuka mipaka ya nchi za Afrika ili kuchochea mageuzi ya uchumi barani Afrika. Mjadala huo rasmi umefanyika kando ya mkutano wa mwaka 2024 wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) ambapo Benki ya CRDB ni miongoni mwa taasisi chache kutoka nchini Tanzania zinazoshiriki.
Mkutano huo mkubwa kwa sekta ya fedha barani Afrika unafanyika jijini Nairobi nchini Kenya kuanzia Mei 27 hadi 31 ukitarajiwa kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 3,000 wakiwamo viongozi wa nchi, viongozi wa taasisi za serikali na taasisi za fedha barani Afrika.
Akizungumza katika mjadala huo rasmi ulioandaliwa kando ya mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kuwa benki hiyo imeendelea na jitihada zake za kujiimarisha nje ya mipaka ya Tanzania huku ikihamasisha taasisi nyingine za fedha nchini Tanzania kufata muelekeo huo kwani taasisi za fedha na hasa mabenki yana mchango mkubwa katika maendeleo ya bara la Afrika.
"Tukiwa benki ya kwanza nchini inayomilikiwa na kuongozwa na wazawa kuvuka mipaka ya nchi na kufungua kampuni tanzu nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, tunajisikia faraja na heshima kubwa kupata nafasi ya kuandaa mjadala huu ambao unalenga kutoa hamasa ya kwa taasisi za fedha katika nchi zetu za Afrika kutanua wigo wa huduma nje ya mipaka ya nchi zetu ili kuchochea mageuzi ya uchumi barani Afrika" alisema Nsekela.
Akiendelea kuchangia katika mjadala huo, Nsekela amesema kuwa safari ya Benki ya CRDB kujitanua nje ya mipaka ya Tanzania ni endelevu ambapo mbali na uwepo wa kampuni tanzu za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, benki hiyo ipo katika hatua za upembuzi yakinifu wa masoko mengine ya Afrika pamoja na kuanzisha ofisi za kimkakati katika baadhi ya nchi za nje ya bara la Afrika.
Naye mmoja kati ya washiriki wa mjadala huo, Mkurugenzi wa Norfund wa Ukanda wa Afrika Mashariki, William Nyaoke ametoa hoja ya kuzitaka serikali za nchi za Afrika kuwa na sera madhubuti zisizobadilika mara kwa mara ili kuzivutia taasisi za fedha kuwekeza nje ya mipaka ya nchi zinapotoka na hivyo kuchochea mageuzi ya uchumi barani Afrika.
Mbali na kushiriki mkutano mkutano wa mwaka 2024 wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) na kuandaa mjadala wenye lengo la kuchochea mageuzi ya uchumi barani Afrika, ujumbe wa Benki ya CRDB ukiongozwa na Nsekela umeweza kufanya mikutano kadhaa na mashirika ya fedha ya kimataifa ikiwamo Afreximbank na African Guarantee Fund (AGF).
Mikutano hiyo ya kimkakati imelenga kuboresha mahusiano kati ya taasisi hizo ambazo tayari ni wabia wa Benki ya CRDB ambapo taasisi hizo zimekua zikiiwezesha benki kutoa mikopo katika sekta ambazo zimekua na uhitaji mkubwa wa uwezeshaji ikiwamo sekta ya kilimo na biashara huku pia sehemu ya fedha hizo zikilenga makundi ya vijana na wanawake. Sambamba na hayo, mikutano hiyo imelenga kutanua mashirikiano na taasisi hizo katika kampuni tanzu za Benki ya CRDB nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
No comments:
Post a Comment