BIL 97.178 KUTUMIKA UJENZI BARABARA YA IFAKARA-MBINGU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 16, 2024

BIL 97.178 KUTUMIKA UJENZI BARABARA YA IFAKARA-MBINGU


Imeelezwa kuwa mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Ifakara hadi Mbingu yenye urefu wa kilomita 62.5 utatumia Bilioni 97.178


Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imebainisha kuwa Mkandarasi wa Kampuni ya M/s Henan Highway Engineering Group Co. Ltd ya kichina imepewa zabuni ya kujenga barabara ya Ifakara-Kihansi yenye urefu wa kilometa 124 sehemu ya kwanza Ifakara-Mbingu ya kilometa 62.5 kwa kiwango cha lami.



Akizungumza mara baada ya kukagua hatua zinazoendelea za kuanza ujenzi wa barabara hiyo mara baada ya mvua kubwa za El-Nino kuanza kupungua Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro Mhandisi Alinanuswe Kyamba amesema kuwa kilio kikubwa cha wananachi ni kupata barabara ya lami ambapo kwa sasa kimepatiwa majawabu kwa serikali ambapo tayari imetoa fedha na mkandarasi yupo eneo la mradi kwa ajiili ya ujenzi huo.


Mhandisi Kyamba amesema kuwa mradi huo utasimamiwa na kitengo cha usimamizi wa miradi cha TANROADS (TECU) na kwa sasa mkandarasi ameanza kufanya matengenezo ili barabara inayotumika sasa ianze kupitika kwani hilo ni jukumu lake kwa mujibu wa mkataba.

Ameeleza kuwa barabara hiyo ni muhimu kwa wananchi kusafirisha bidhaa mbalimbali ikiwemo za kilimo kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo mkoa wa Morogoro pamoja na mkoa wa Njombe kupitia Ifakara, Mlimba, Kihansi hadi Makambako Mkoani Njombe.

Mhandisi Kyamba amesema kuwa Mradi huo wa ujenzi wa barabara ya Ifakara-Mbingu ni wa miezi 30 ambao umeanza tarehe 8 Disemba 2023 na unatarajiwa kumalizika ifikapo tarehe 8 juni 2026.

Naye Mhandisi Ntwale Lukas ambaye ni Fundi Sanifu Mkuu wa TANROADS Mkoa wa Morogoro amesema kuwa baada ya mvua za El-Nino kupungua tayari kwa sasa magari yameanza kusomba vifusi ili kurekebisha maeneo yote korofi ili kurudisha mawasiliano ya barabara.

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Igima, kijiji cha Lufufu wameishukuru serikali inayoongozwa na Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuanza kujenga barabara hiyo kwakuwa itaharakikisha maendeleo yao ya kijamii na kiuchumi hasa usafirishaji wa uhakika wa mazao hususani mpunga (mchele) na ndizi.

Wamesema kukamilika kwa ujenzi wake kutapunguza gharama za usafiri na usafirishaji wa mazao hayo kwenda kwenye masoko ya mjini na kuongeza kwa thamani ya mazao ya wakulima fofauti na sasa kutokana na kuwepo changamoto za miundombinu ya barabara.


No comments:

Post a Comment