Serikali ya mpito ya Burkina Faso imeongezwa muda kwa miaka mitano kufuatia kupitishwa kwa katiba iliyofanyiwa marekebisho katika mkutano wa kitaifa wa mashauriano.
Kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi Kapteni Ibrahim Traoré alitia saini mkataba huo uliorekebishwa mjini Ouagadougou siku ya Jumamosi, na kuongeza muda wake wa kukaa madarakani zaidi ya kipindi cha awali cha miezi 21.
Marekebisho makubwa katika mkataba huo yamemtambulisha Kapteni Ibrahim Traoré kama Rais wa Burkina Faso na kiongozi mkuu wa jeshi la kitaifa kwa muda wa serikali ya mpito, kuanzia Julai 2, 2024.
Washiriki katika mkutano wa mpito wa kitaifa pia walikubali kwamba Traoré , Waziri Mkuu, na Rais wa Bunge la Kutunga Sheria watashiriki uchaguzi ujao mwishoni mwa kipindi cha miezi 60 serikali ya mpito itakapomaliza muda wake.
Maamuzi yaliyotolewa wakati wa mashauriano ya kitaifa yalifanyika haraka, na baadhi ya ripoti za vyombo vya habari za ndani zikionyesha kutokuwepo kwa vyama vya siasa mwanzoni mwa mkutano.
Burkina Faso imekuwa chini ya utawala wa kijeshi tangu 2022, ikikabiliwa na changamoto katika kudhibiti waasi wa Kiislamu wanaohusishwa na al Qaeda na Islamic State.
No comments:
Post a Comment