Watu 12 wamejeruhiwa kutokana na msukosuko kwenye ndege kutoka Doha kuelekea Dublin.
Ndege hiyo aina ya Boeing 787-9 dreamliner ilikumbwa na misukosuko ilipokuwa ikisafiri kwenye anga ya Uturuki, mwendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Dublin, DAA, alisema.
Ilipotua muda mfupi kabla ya saa 13:00 kwa saa za huko, ndege ya Qatar Airways nambari QR107 ilipokelewa na huduma za dharura wakiwemo polisi wa uwanja wa ndege na maafisa wa zima moto.
Abiria sita na wahudumu sita wameripoti kujeruhiwa.
"Timu ya Uwanja wa Ndege wa Dublin inaendelea kutoa usaidizi kamili kwa abiria na wafanyakazi wa ndege," msemaji wa DAA aliongeza.
Tukio hilo linafuatia kifo cha Muingereza mwenye umri wa miaka 73 kwenye ndege iliyokuwa ikielekea Singapore ambayo ilikumbwa na misukosuko mikali mapema wiki hii.
Zaidi ya watu 100 walijeruhiwa, 20 kati yao wako katika uangalizi maalum na majeraha ya uti wa mgongo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Singapore, Goh Choon Phong aliomba radhi, na kutoa "pole zake nyingi kwa kila mtu aliyeathiriwa" na "msukosuko mkubwa wa ghafla".
Serikali ya Singapore imeahidi uchunguzi wa kina.
No comments:
Post a Comment