CHIKOTA ASHAURI MAMBO MATANO KWENYE ZAO LA KOROSHO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 3, 2024

CHIKOTA ASHAURI MAMBO MATANO KWENYE ZAO LA KOROSHO

Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota,akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka 2024/25 bungeni jijini Dodoma.


Na Mwandishi Wetu, DODOMA


Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan namna anavyothamini sekta ya kilimo na dhamira ya kuwakomboa wakulima kwa kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka Sh.Bilioni 900 hadi Trilioni 1.24.


Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka 2024/25 bungeni, Chikota amesema maono hayo ya Rais yanatokana na ubunifu wa watendaji wa Wizara ya Kilimo kwa kuanzisha programu zinazowakomboa wakulima.


Chikota akizungumza tasnia ya korosho, amesema katika mkutano wa tathmini ya zao hilo Mwaka Jana walikubaliana iundwe timu ya wataalamu ya kuangalia mnyororo wa thamani wa korosho ili kubaini changamoto na kutoa mapendekezo kwa Wizara ili kutafuta ufumbuzi.


"Nimpongeze Waziri aliunda timu ya watu makini na imekuja na ripoti ambayo Wizara imeanza kufanyia kazi niipongeze kwa kazi kubwa iliyofanya ya kuchambua kuanzia uzalishaji, uvunaji na uongezaji thamani,"amesema.


Amesema katika mfumo wa uuzaji korosho timu hiyo ilibaini kuna changamoto na malalamiko na kupendekeza msimu huu uwepo mfumo wa TMX ambao Serikali imekuja na maamuzi hayo.


"Wakulima wa korosho wamefurahi uamuzi huu wanachotaka ni bei nzuri ya korosho sokoni na wanufaike na Kilimo chao, nashauri wakati TMX inaingia iangalie changamoto zilizojitokeza wakati tunatumia kwenye zao la ufuta, changamoto ya kwanza wakati ule ilikuwa wahusika kutokuwa karibu na wakulima kitu ambacho tunatarajia msimu huu TMX watakuwa na utaratibu wa kuweka Ofisi jirani na wakulima ili kutatua changamoto zinazojitokeza."


Amesema timu hiyo ilibaini tozo nyingi kwenye korosho zinazomuumiza mkulima sokoni na kuomba Waziri kwa kuwa serikali itarudisha export levy asilimia 50 na hivyo kutoa asilimia 100 kwa zao hilo ni muda wa kupitia kuondoa tozo zingine ili mkulima apate bei nzuri sokoni.


"Kwa mapendekezo yangu tozo ambazo tunaweza kuanza nazo ni zile tunazopeleka kwenye Taasisi zinazopata fedha kwa utaratibu mwingine, kwa mfano tozo ya TARI tumeona wanachukua kwenye pamba Sh.Bilioni mbili, nashauri ni vyema kwenye korosho nasi tukatenga fedha na sio kuwakata wakulima kwa kila kilo sh.25 ukipiga hesabu Kila Mwaka zinatolewa zaidi ya Sh.Bilioni sita kwenda TARI."


Ametaja tozo nyingine ni inayopelekwa Bodi ya Korosho na kwamba ni Taasisi ya umma inayoweza kujiendesha kwa ruzuku za kawaida ya serikali kama ilivyo kwa nyingine na hakuna sababu mkulima kuchangia Sh.25 kwa kilo kwa ajili ya uendeshaji wa Bodi hiyo na kushauri pia tozo hiyo iondolewe.


"Soko la awali limekuwa chanzo cha vurugu ni muda muafaka kama ilivyopendekezwa na timu wawezeshwe wabanguaji wa ndani, naomba katika soko la awali utolewe mwongozo mpya kuhakikisha halivurugi minanda wakati wa msimu,"amesema


Aidha, amesema timu hiyo iliangalia suala la uongezaji thamani katika kongani ya ubanguaji korosho ya Malanje na kwamba ni wakati wa serikali kujikita kwenye korosho karanga na si kupeleka korosho ghafi nje na itasaidia kupata bei nzuri kwa mkulima wa korosho.


"Wizara imeshapeleka zaidi ya sh.bilioni tano kwa Bodi kukamilisha mradi huu naomba iongeze kasi ya utekelezaji ili kongani ianze kufanya kazi, na kwenye maeneo ambayo Bodi imetwaa ardhi wananchi walipwe fidia zao kwa wakati na ujenzi ianze,"amesema.


Amempongeza serikali kwa kutoa pembejeo bure kwa wakulima wa korosho kwa miaka mitatu sasa na kuomba Wizara iimarishe usajili wa wakulima ili kurahisisha zoezi hilo.

No comments:

Post a Comment