Muonekano wa Soko jipya linalojengwa Katesh kwa ajili ya waathirika wa maafa Hanang Mkoani Manyara. (PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU) |
NA. MWANDISHI WETU
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba 108 za waathirika wa maafa ya maporomoka ya mawe, tope na miti kutoka mlima Hanang’ yaliyotea Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara mwishoni mwa mwaka Jana, 2023.
Dkt. Yonazi amefanya ziara hiyo mwishoni mwa wiki ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza uwekaji wa mifumo ya anwani za Makazi katika nyumba hizo zitakazoonesha namba za nyumba na vibao vyenye majina ya mitaa kurahisisha utambuzi wa makazi na wakazi husika ili kurahisisha ufikishaji wa huduma na bidhaa mahali stahiki na kuchagiza maendeleo kwa wananchi hao.
Dkt. Yonazi ametoa maagizo hayo ya kuweka anwani za makazi kwa kuzingatia umuhimu wake katika nyumba hizo zinazojengwa katika eneo la Gidagamowd lililopo katika Kitongoji cha Waret Wilayani Hanang mkoani humo.
Alisema kuwa Serikali imetenga eneo la ekari 100 ambapo jumla ya viwanja 269 vimepimwa ambapo kati ya hivyo, viwanja 226 ni makazi pekee, viwanja 26 ni makazi na biashara na viwanja 17 ni maeneo ya huduma za kijamii.
Aidha amewata wakandarasi kukamilika utekelezaji wa mradi husika kwa wakati na kuzingatia ubora unaotakiwa.
“Mradi ukamilike kwa wakati kama ilivyokubalika yaani ndani ya siku tisini na uendane na thamani ya fedha itakayotumika pamoja na hilo endeleeni kushirikiana na wenyeji wa eneo hili ili kuimarisha mahusiano na wazawa,” alisisitiza Dkt. Yonazi
Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo Kaimu Operesheni Kamanda Luteni Kanali Ashraf Hassan ameahidi kuhakikisha kuwa maelekezo yaliyotolewa na Dkt. Yonazi yanafuatwa ili ujenzi ukamilike kwa wakati.
Luteni Kanali Ashraf amemueleza Katibu Mkuu kuwa ujenzi huo wa nyumba 73 umefikia asilimia 40, na unajengwa kwa kuzingatia vigezo vya ubora uliokusudiwa na Serikali.
"Tumefurahi kutembelewa na Katibu Mkuu Dkt. Yonazi ambaye ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi, na sisi tunamuahidi kuwa ujenzi huu utakamilika kwa wakati lakini pia kwa kuzingatia viwango vya ubora vilivyoelekezwa" amesema Luteni Kanali Ashraf
Akieleza faida za mradi wa ujenzi amesema kuwa umesaidia kutoa ajira kwa wenyeji, biashara ndogondogo hasa za mama lishe, kukuza uchumi wa wakazi wa Katesh pamoja na kuimarisha mahusiano na wakazi wa maeneo hayo pamoja na uboreshwaji wa miundombinu ya barabara, maji na umeme katika maeneo ya mradi.
Disemba 3, 2023 Wilaya ya Hanang’ ilikubwa na maafa yaliyosababishwa na maporomoko ya tope, miti na mawe Wilayani yaliyouwa zaidi ya watu 80 huku mamia wengine wakiachwa bila makazi.
Serikali iliratibu masuala yote ya menejimenti ya maafa ikiwa ni pamoja na hatua ya kurejesha hali ambapo kwa sasa zinajengwa nyumba 108 za waathirika wa maafa hayo, ambapo nyumba 73 zinajengwa na Serikali kwa kutumia SUMAJKT na zingine 35 zinajengwa na Chama cha Msalaba Mwenkundu (Tanzania Red Cross Society) kwa kushiriana na wadau mbalimbali ili kurejesha makazi kwa wananchi hao.
No comments:
Post a Comment