MBUNGE AHOJI MFUMO MZURI WA KURAHISISHA KUTOA MSAMAHA WA KODI KWA WAKANDARASI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, May 20, 2024

MBUNGE AHOJI MFUMO MZURI WA KURAHISISHA KUTOA MSAMAHA WA KODI KWA WAKANDARASI


Na Saida Issa,Dodoma

SERIKALI imesema kuwa Msamaha wa kodi kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya kimkakati ya serikali unatolewa kwa mujibu wa kifungu cha Sita (6) cha Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani(VAT) kama ilivyofanyiwa maboresho na sheria ya Fedha ya Mwaka 2021.

Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha Hamad Chande alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Msalala Iddi Kassim Iddi alipouliza Je, Serikali ina mpango gani wa kurahisisha mfumo mzuri wa kutoa msamaha wa kodi kwa Wakandarasi wanaojenga barabara Halmashauri ya Msalala.

Alisema kuwa maboresho ya sheria hiyo yalilenga kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utoaji wa msamaha wa kodi, ambapo awali mamlaka ya kutoa msamaha yalikuwa chini ya Waziri wa Fedha, aidha, kwa marekebisho hayo, Mamlaka ya kutoa msamaha yakakasimishwa kwa Kamishna Mkuu wa TRA.

"Mheshimiwa Spika, kutokana na maboresho ya sheria, Serikali kupitia TRA, ilianzisha kitengo maalumu kwa ajili ya kushughulikia misamaha ya kodi ya Ongezeko la Thamani, 

Kuanzishwa kwa kitengo hicho kumesababisha kuwa na muda mfupi zaidi wa kushughulikia maombi ya msamaha wa kodi hiyo ukilinganisha na wakati wa awali kabla ya maboresho,"alisema.

Aidha alisema kuwa katika jitihada za kuongeza ufanisi na kutoa msamaha wa kodi ndani ya muda mfupi, Serikali ilianzisha mfumo wa kieletroniki wa kuwasilisha maombi hayo TRA (Tax Exemption Mangement System).

No comments:

Post a Comment