RAIS WA ZAMANI WA ZAMBIA ADAI ANAZUILIWA NYUMBANI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 23, 2024

RAIS WA ZAMANI WA ZAMBIA ADAI ANAZUILIWA NYUMBANI.

Kiongozi huyo wa zamani ameamua kurejea kwa kishindo katika siasa kabla ya uchaguzi wa 2026.


Rais wa zamani wa Zambia Edgar Lungu amesema kuwa "kiuahlisia amewekwa katika kizuizi cha nyumbani", akiwashutumu polisi kwa njama ya kumshikilia kwa nguvu "bila sababu".


Bw Lungu alisema polisi walikuwa wanajipanga kumkamata usiku kutoka katika makazi yake katika mji mkuu, Lusaka.


Haya yanajiri siku chache baada ya kiongozi huyo wa zamani kunukuliwa akisema huenda kukawa na mabadiliko ya serikali kabla ya uchaguzi mkuu wa 2026.


Mkuu wa polisi Graphael Musamba alisema Bw Lungu ataitwa kufafanua kauli yake, vyombo vya habari vya nchini humo viliripoti.


Bw Lungu alitangaza kurejea katika siasa Oktoba mwaka jana, na kusababisha serikali kumfutia marupurupu yake ya kustaafu.


Alikuwa amestaafu siasa baada ya kushindwa na Hakainde Hichilema katika uchaguzi mwaka 2021.


Kiongozi huyo wa zamani amekuwa akiishutumu serikali kwa kumuonea yeye na wanachama wa chama chake cha Patriotic Front (PF) kumzuia asirejee kwenye siasa.


Mkewe Esther Lungu, ameshtakiwa kwa ufisadi unaohusisha kesi za wizi wa magari na hati miliki.


Anakanusha madai hayo. Serikali imekana kumlenga Bw Lungu na kumtaka ampe mrithi wake muda wa kutimiza ahadi zake za kampeni.


Siku ya Jumatano, Bw Lungu alisema amekuwa akikabiliwa na vitendo kadhaa vya ukiukaji katiba kutoka kwa serikali baada ya kuondoka madarakani.


Alidai polisi walikuwa chini ya maagizo ya "kunivizia usiku, kuniteka nyara, kunidhalilisha, na kuniweka kizuizini kwa nguvu kama mhalifu mkali".


“Ninavyofahamu, sijafanya uhalifu wowote ambao ungeidhinisha serikali, kupitia polisi, kuanza kupanga njama dhidi yangu kwa njia hii,” Bw Lungu aliongeza.


Haijabainika ikiwa bado kuna polisi nyumbani kwake siku ya Alhamisi na polisi hawakujibu ombi la BBC kuhusu suala hilo.


Lakini afisi ya rais imejitetea huko nyuma kuwa inaheshimu haki za binadamu na haiingilii shughuli za polisi.


Akihudhuria ibada ya kanisa Jumapili iliyopita, Bw Lungu alionya kuhusu mabadiliko ya utawala kabla ya uchaguzi ujao, akisema "mtoto anaweza kuzaliwa kabla ya miezi tisa".


Waziri wa Habari Cornelius Mweetwa alisema serikali "inachunguza kwa makini" matamshi ya Bw Lungu.


Haya yanajiri siku chache baada ya polisi kuonya kuwa Bw Lungu anakabiliwa na hatari ya kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa "kujihusisha na shughuli zinazovuruga utulivu na usalama wa umma".

No comments:

Post a Comment