Na Mwandishi Wetu, Beijing
Kampuni ya huduma za Televisheni ya nchini China ya StarTimes itakuwa tayari kurusha filamu ya “Amazing Tanzania” kupitia Tv na mitandao yao ya kijamii ili kuwafikia watalii wengi zaidi kutoka nchini humo kutembelea Tanzania.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti na Mwanzilishi wa StarTimes Group, Bw. Pang XinXing, wakati wa ziara ya wajumbe wa Kamati ya Rais ya Kuitangaza Tanzania wakiongozwa na Mwenyekiti ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hasssan Abbasi, walipotembelea makao makuu ya taasisi hiyo Beijing nchini China leo Mei 13, 2024.
“Kutokana na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya China na Tanzania dna kupitia uwekezaji wetu wa StarTimes nchini Tanzania na nchi nyingine za Afrika, tutatoa ushirikiano wa kila namna ili filamu ya Amazing Tanzania iwafikie watazamaji wengi zaidi wa Kichina duniani,” alisema Bw. Pang XinXing ambaye pia wataalamu wake ni sehemu ya magwiji wa kutayarisha filamu walioshiriki kuiandaa filamu hiyo.
Dkt. Abbasi katika ziara hiyo ambapo pia walikutana na baadhi ya Watanzania wanaofanya kazi mbalimbali za habari na kuingiza sauti (dubbing) kwenye makao makuu hayo ya StarTimes aliambatana na wajumbe wengine wa Kamati hiyo akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Fatma Mabrouk na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Anderson Mutatembwa.
Filamu ya Amazing Tanzania itazinduliwa rasmi Mei 15, 2024 hapa jijini Beijing China katika hafla ambapo pia msanii mashuhuri hapa China aliyeshiriki filamu hiyo Jin Dong atahutubia.
No comments:
Post a Comment