Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb), ameitaka Wizara ya Ujenzi kukamilisha maboresho yaliyotolewa na Wabunge kuhusu mkakati wa kuongeza ushiriki wa wazawa kwenye utekelezaji wa miradi ya ujenzi ili Bunge liweze kuja na mkakati wa pamoja kati yake na Serikali.
Zungu ameyasema hayo jijini Dodoma Mei 11, 2024 wakati wa Semina iliyoandaliwa na Wizara ya Ujenzi kwa Waheshimiwa Wabunge ili kuwajengea uelewa wa mikakati ya ushiriki wa Wakandarasi na Washauri Elekezi Wazawa kwenye miradi.
“Hauwezi kufanikiwa bila kufanya makosa, na kama utaogopa kufanya makosa hutaweza kufanikiwa, makosa mengi mmefanya na mmeainisha sasa mnataka kwenda kuyafanyia kazi na kuleta maendeleo ya Taifa letu na kwa hili nawapongeza Serikali”, amesema Mheshimiwa Zungu.
Aidha, Naibu Spika Zungu ameeleza kuwa kutokana na changamoto ya fedha za Serikali kwenda nje kwa miradi inayotekelezwa na Wakandarasi kutoka nje ya nchi, Serikali imeona umuhimu wa kuweka mikakati madhubuti wa kuweza kuwanufaisha Wakandarasi na Washauri Elekezi wazawa kwa kuwashirikisha kwenye utekelezaji wa miradi ya ujenzi nchini.
Ametoa rai kwa Taasisi za Kifedha nchini kuangalia namna ya kupunguza riba kwani riba hizo ndio zinazopelekea kurudisha nyuma Wakandarasi na Makampuni ya Wakandarasi ambao huchukua mikopo kwenye Taasisi hizo.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Selemani Kakoso (Mb), ameitaka Wizara ya Ujenzi kuhakikisha inasimamia wazawa kutekeleza miradi inayotekelezwa kwa ubora na kwa wakati ili iwe mifano katika maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa ameeleza kuwa tathimini iliyofanyika katika kipindi cha miaka 10 kuanzia Mwaka 2013 hadi 2023 inaonesha kuwa miradi yenye thamani ya Shilingi Trilioni 61.64 ilisajiliwa na kutekelezwa nchini ambapo kati ya hiyo wazawa wametekeleza asilimia 38.5 na asilimia 40 ilitekelezwa na Wakandarasi wa Nje ambao kwa ujumla wake hawazidi 500, hivyo inaonesha kuwa miradi yenye thamani kubwa mingi imetekelezwa na Wakandarasi wa Nje.
Ameeleza faida za mkakatai huo kuwa utasaidia kuongeza wigo wa ajira katika Sekta ya Ujenzi, kujenga, kukuza ujuzi na uzoefu na hivyo kutekeleza miradi mikubwa pamoja na kuokoa fedha za kigeni na kuhakikisha fedha hizo zinabaki nchini.
“Mkakati huu unakwenda kujibu changamoto ambazo zimekuwa zikiwasilishwa na wazawa Serikalini na ni muda sahihi wa Wizara ya Ujenzi kushirikiana na Wizara nyingine kuhakikisha mpango mkakati huu unafanikiwa”, amesema Bashungwa.
Mkakati wa kuongeza ushiriki wa wazawa kwenye utekelezaji wa miradi ya ujenzi una lengo la kuwajengea uwezo hatua kwa hatua Wakandarasi, Washauri Elekezi na Watalaam wazawa ili waweze kutekeleza miradi mikubwa ya ndani na hatimaye kushindana kimataifa.
No comments:
Post a Comment