Na Happiness Shayo
Wizara ya Maliasili na Utalii imeomba kuidhinishiwa Bajeti ya jumla ya Shilingi Bilioni 348.12 (bilioni mia tatu arobaini na nane milioni mia moja ishirini na tano laki nne na elfu kumi na tisa) kwa matumizi ya Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema hayo leo Mei 31/05/2024 wakati wa akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii Bungeni jijini Dodoma.
Amesema kati ya fedha hizo zilizoombwa, Shilingi 250,884,083,000 (bilioni mia mbili hamsini milioni mia nane themanini na nne na elfu themanini na tatu) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 97,241,336,000 (bilioni tisini na saba milioni mia mbili arobaini na moja laki tatu na elfu thelathini na sita) ni za Miradi ya Maendeleo.
Fedha za Matumizi ya Kawaida zinajumuisha Shilingi 125,366,391,000 (bilioni mia moja ishirini na tano milioni mia tatu sitini na sita laki tatu na elfu tisini na moja) za Mishahara na Shilingi 125,517,692,000 (bilioni mia moja ishirini na tano milioni mia tano kumi na saba na laki sita na elfu tisini na mbili) za Matumizi Mengineyo. Fedha za Miradi ya Maendeleo zinajumuisha Shilingi 18,074,661,000 (bilioni kumi na nane milioni sabini na nne laki sita na elfu sitini na moja) fedha za ndani na Shilingi 79,166,675,000 (bilioni sabini na tisa milioni mia moja sitini na sita laki sita na elfu sabini na tano) fedha za nje.
Waziri Kairuki amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa kipaumbele Sekta hiyo kwa kufanya uwekezaji mkubwa ambao umekuwa na matokeo chanya yenye mchango mkubwa katika kuimarisha uhifadhi, kuongeza watalii na mapato hivyo kuleta manufaa makubwa kwa uchumi wa Nchi yetu.
Amesema pamoja na mafanikio mengi yaliyopatikana mafanikio matatu makubwa yaliyotokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika Sekta ya Maliasili na Utalii chini ya uongozi wake mahiri ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watalii ambapo idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kwa asilimia 96 kutoka watalii 922,692 Mwaka 2021 hadi watalii 1,808,205 Mwaka 2023.
Aidha, idadi ya Watalii wa Ndani waliotembelea vivutio vya utalii imeongezeka kwa asilimia 152 kutoka watalii 788,933 Mwaka 2021 hadi kufikia watalii 1,985,707 Mwaka 2023. Hii ni rekodi kubwa haijapata kufikiwa katika Nchi yetu.
Ameongeza kuwa pia kupitia Serikali ya Awamu ya Sita kumekuwa na ongezeko la mapato yatokanayo na shughuli za utalii ambapo yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.3 Mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 3.4 Mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 161 kwa watalii wa kimataifa.
Waziri Kairuki amesema mapato yatokanayo na utalii wa ndani yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 46.3 Mwaka 2021 hadi Shilingi bilioni 175.3 Mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 279. Aidha, ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali uliongezeka kutoka Shilingi 397,428,671,968 Mwaka 2020/2021 hadi Shilingi 680,150,218,337 Mwaka 2022/2023. Vilevile, kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 kuanzia Julai 2023, hadi kufikia Aprili 2024, Wizara imekusanya jumla ya Shilingi 750,992,839,479.75 sawa na asilimia 97.12 ya lengo la makusanyo. Makusanyo hayo pia ni rekodi ya juu ya mapato kuwahi kuwekwa katika Sekta hizo Nchini.
Waziri Kairuki amefafanua kuwa pia kuimarika kwa ulinzi na usimamizi wa rasilimali za wanyamapori kumeiwezesha Tanzania kuendelea kuongoza barani Afrika kwa kuwa na simba wapatao 17,000; nyati 225,000; na chui 24,000. Sambamba na hilo, takwimu zinaonesha kuwa faru wameongezeka kutoka 163 Mwaka 2021 hadi 252 Aprili, 2024.
No comments:
Post a Comment