Serikali imetoa jumla ya Shilingi Bilioni 136.2 kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS) na Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), kwa ajili ya kurejesha hali ya awali ya miundombinu ya barabara na madaraja yaliyoharibiwa kwa kiasi kikubwa na janga la mvua za El Nino.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba Bungeni jijini Dodoma Mei 13, 2024 wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali 2024/2025.
Dkt. Mwigulu amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa.
Dkt. Mwigulu amezielekeza Taasisi zote zinazohusika na ujenzi wa miundombinu kuhakikisha zinafanya usanifu wa miradi kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi.
Ameeleza kufuatia mvua za El-Nino zilizonyesha nchini kuanzia Septemba, 2023 pamoja na kimbunga Hidaya, barabara mbalimbali za kitaifa katika mikoa 26 zimeathirika ambapo barabara 68 zilikuwa zimejifunga, barabara 106 zilikuwa zinapitika kwa shida na barabara 168 ziliathirika lakini zinaendelea kupitika kwa shida baada ya kufanyiwa matengenezo ya dharura.
“Maeneo yaliyoathirika katika barabara hizo yanakadiriwa kufikia kilometa 520 na kwa upande wa madaraja na makalavati yapatayo 189 yalikuwa yamekatika na mengine kuharibika vibaya”, ameeleza Dkt. Mwigulu.
Aidha, Dkt. Mwigulu ameongeza kuwa tathmini iliyofanyika inaonesha gharama za kurejesha miundombinu hiyo ni shilingi trilioni 1.07 ambapo kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 728 ni kwa ajili ya kufanya matengenezo ya kurejesha miundombinu ya barabara ili zirudi katika hali yake ya awali na shilingi bilioni 158 ni kwa ajili ya matengenezo ya dharura ili barabara hizo ziweze kupitika.
Amefafanua kuwa shilingi bilioni 184.14 ni kwa ajili kurejesha miundombinu iliyoathiriwa na kimbunga Hidaya.
No comments:
Post a Comment