SERIKALI kupitia Mfumo wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeingia makubaliano na Kampuni ya simu ya Vodacom kwa ajili ya ujenzi wa mnara katika kata ya Makuro utakaohudumia vijiji vya Ghalunyangu na Mwalala.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi MaryPrisca Mahundi alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Singida Kaskazini Abeid Ramadhani alipouliza Je, Serikali ina mpango gani wa kuvipatia mawasiliano ya simu Vijiji 13 na Kata 8 za Muchunga, Ngimu, Makuro, Mudida, Ughandi, Msisi, Msange na Mgori.
"Mheshimiwa Spika, Kwa kata za Ngimu kijiji cha Lamba, Kata ya Msisi vijiji vya mnunguna na Mkwae, Kata ya Msange vijiji vya Muriga na Endeshi UCSAF imeingia makubaliano na TTCL kupeleka huduma za mawasiliano katika Kata tajwa,"alisema.
Aidha alisema kuwa UCSAF imeingia pia makubaliano na Vodacom kwa ajili ya kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata Ughandi (kijiji cha Misinko).
Kwa upande wa Kata ya Mudida kijiji cha Migugu UCSAF imeingia makubaliano na Kampuni ya simu ya Halotel.
"Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa miradi hii, Serikali kupitia UCSAF itafanya tathmini ya hali ya mawasiliano katika kata hizo na kuchukua hatua stahiki kulingana na upatikanaji wa fedha,"alisema.
No comments:
Post a Comment