* Ni Kamishna Mkuu wa TRA aliyevunja rekodi ya makusanyo ya kodi za Serikali
* Genge la wakwepakodi likishirikiana na vigogo wala rushwa limewalipa wahuni kwenye mitandao wamchafue bosi wa TRA
* Wahuni waanzisha kampeni chafu kutaka Kidata ang'olewe TRA ili awekwe kamishna wao mla rushwa
Juni 24, 2024
Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam
Kampeni chafu imeanzishwa kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA), Alphayo Kidata, na genge la wakwepa kodi ili kujaribu kumchafua Kamishna huyo.
Genge hilo limewalipa wahuni wasambaze ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, ikiwemo X (zamani ikijulikana kama Twitter), Instagram, Facebook na WhatsApp kumchafua Kidata.
Lengo la kampeni hiyo chafu ni kuibua taharuki kwenye jamii dhidi ya Kamishna Mkuu wa TRA na kumshawishi Rais Samia Suluhu Hassan amng'oe kwenye nafasi hiyo.
"Hili genge la wakwepa kodi tayari limeandaa mtu wao ambaye wamempendekeza kwa Rais awe Kamishna Mkuu wa TRA ili waweze kufanya upigaji wao wa kodi za serikali," alisema afisa mmoja aliye karibu na Serikali.
"Unajua Kamishna Kidata hataki mchezo na hacheki na mtu kwenye ukusanyaji wa kodi za serikali. Kidata amekuwa ni mwiba mkali kwa wakwepa kodi na vigogo wala rushwa serikalini ambao sasa wameungana kumpiga vita."
Wachambuzi wa mawasiliano ya mitandao ya kijamii wamebaini kuwa kampeni hiyo chafu dhidi ya Kidata imeanza siku kadhaa sasa.
Kampeni hiyo chafu ilianza kwa kusambazwa kwa taarifa za kughushi (fake news) kuhusu mgomo wa wafanyabiashara wa Kariakoo na sehemu nyingine nchini kuhusu masuala ya kodi.
Taarifa hizo za kughushi zimetumika kusambaza ujumbe kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya Kidata ili kujaribu kumchafua kwenye jamii.
"Kidata kavunja rekodi zote za ukusanyaji wa kodi, hana makosa, atoke kwa merit (sifa) nyingine sio jumba bovu. Nchi hii ijifunze kuheshimu wataalamu. Sheria mnatunga wenyewe TRA wanatekeleza sasa mnawaangushia jumba bovu," alisema Fred Kavishe kupitia mtandao wa X.
Dkt. Zakayo Mmbaga naye akauliza "Nani tena kawalipa kumchafua Kidata?"
Injinia Aloyce Msaki akasema: "Ninavyojua mimi TRA inafanya kazi kwa mujibu wa sheria zinazopitishwa na Bunge. Sasa kosa la Kidata ni lipi?"
Naye Jeff Msangi alisema kuwa wahuni sasa wamepanga "kumtoa sadaka" Kidata.
Wachambuzi wa siasa nchini wamesema kuwa kuna genge la vigogo wala rushwa kwenye serikali ya Rais Samia ambalo limekuwa likifanya kampeni chafu dhidi ya watumishi wa umma waaminifu.
Genge hilo pia limehusishwa na kampeni chafu iliyomng'oa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, na wateule wengine waaminifu na waadilifu wa Serikali.
"Anayewatuma kwenye hii kampeni kakosa akili na maarifa kabisa! Haya majitu yanakwepa kodi na huo ni ukweli! Yaani (Kidata) must Go! Where? Watu hawalipi kodi wakishughulikiwa wanaanza kutoa milio. Nchi haiwezi kuendeshwa hivyo," Amesema Kigogo2014, mtumiaji maarufu wa mtandao wa X.
Kidata ambaye sasa anapigwa vita na wahuni amevunja rekodi ya makusanyo ya kodi za serikali kwa Makamishna Wakuu wote waliopita TRA.
Takwimu za Serikali zinaonesha kuwa kwa mwezi Desemba 2023 peke yake, TRA chini ya uongozi wa Kidata ilivunja rekodi ya makusanyo ya kodi za serikali kwa kukusanya Shilingi trilioni 3.05, ambayo ni sawa na asilimia 103 ya lengo.
Alipoteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa Kamishna Mkuu wa TRA, Kidata alipandisha makusanyo ya kodi kutoka wastani wa Shilingi bilioni 700-800 kwa mwezi mwaka 2016/2017, hadi kufikia wastani wa Shilingi trilioni 1.2-1.5.
Na sasa hivi wastani wa ukusanyaji wa kodi umezidi Shilingi trilioni 2 kwa mwezi chini ya uongozi wa Kidata.
Uongozi wake huu wa kutocheka na wakwepa kodi na mafisadi umemfanya Kidata achukiwe na vigogo wala rushwa ambao wanahusika na kampeni hii chafu ya kwenye mitandao ya kijamii dhidi yake.
No comments:
Post a Comment