WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watendaji wote wanaohusika na sera na mipango katika Serikali Kuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wahakikishe kuwa mipango na maamuzi yote yanayohusu maendeleo ikiwemo utoaji wa huduma kwa wananchi yanazingatia matokeo ya Sensa ya mwaka 2022.
Amesema hayo jana (Jumamosi, Juni 22, 2024) wakati wa hafla ya uzinduzi ripoti ya Kidemografia, Kijamii, Kiuchumi na Mazingira zinazotokana na Sensa ya Watu na Makazi na Sensa ya Majengo ya Mwaka 2022. Hafla hiyo imefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam.
Amesema kuwa matokeo hayo ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa kwa kuwa yanatoa fursa kwa nchi kuendelea kutambua kwa kina hali za kidemografia, kiuchumi, kijamii na mazingira pamoja na hali ya makazi. “Ripoti hizi zina mchango mkubwa katika kutunga na kuhuisha sera mbalimbali zinazohusiana na masuala ya ustawi wa wananchi ikiwemo uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.”
Waziri Mkuu amesema kwa upande wa sekta ya nishati, matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia yameongezeka hapa nchini ambapo, kaya zinazotumia umeme kwa ajili ya kupikia zimeongezeka kutoka asilimia 1.6 mwaka 2012 hadi asilimia 4.3 mwaka 2022 na gesi kutoka asilimia 0.9 mwaka 2012 hadi asilimia 9.4 mwaka 2022.
Amesema kuwa Serikali inasisitiza kuwa matokeo ya Sensa yatumike kikamilifu katika kubaini na kutatua changamoto zinazoikabili jamii kwa namna ambayo ni endelevu. “Nirudie kusisitiza kuhusu umuhimu wa matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi katika ngazi zote za utawala wakati tunapopanga mipango na programu za maendeleo ya wananchi”.
Ameongeza kuwa kupitia utekelezaji wa Sensa ya kidijitali ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi ya Mwaka 2022, Tanzania imetoa mchango wa uzoefu wake katika kufanikisha sensa za nchi nyingine Kikanda na Kimataifa.
“Kimataifa Tanzania imeshaalikwa mara kadhaa na Umoja wa Mataifa kutoa uzoefuwake katika utekelezaji wa Sensa ya kidijitalikatika kuzisaidia nchi nyingine ambazo zilikuwa zinajiandaa kufanya Sensa zao katika Mzunguko wa miaka ya 2020 ya Umoja wa Mataifa wa Kufanya Sensa, ambao ulianza mwaka 2015 na utaisha mwaka 2024.”
Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar na Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla (MBM) alisemaSensa ya watu na makazi ya 2022 ikifanywa na JMT chini ya Samia na Mwinyi imekuwa Sensa ya Mfano hivyo hivyo wataalam wafanye tafsiri ya takwimu za Sensa kwa maslahi ya taifa letu.
No comments:
Post a Comment