Tunduma-Songwe
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amesema Wizara ya Maji tayari imeshaanza kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutekeleza Mradi mkubwa wa Maji wa Kimkakati wa Kutoa maji kutoka chanzo cha Mto Momba kwa ajili ya kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika Mji wa Tunduma pamoja na maeneo mengine ya Mkoani Songwe.
Waziri Aweso ameyasema hayo Leo Julai 18 katika Ziara ya Mhe. Rais alipokuwa akiwasalimia wananchi waliojitokeza kwa wingi kumpokea katika Mji wa Tunduma ambapo Mhe. Aweso ameahidi mbele ya Rais Samia kabla ya kufika mwezi wa 8 wizara itamkabidhi rasmi Mkandarasi Mradi huo.
Mji wa Tunduma kwa muda mrefu umekua na changamoto kubwa ya Maji kutokana na kukosekana kwa vyanzo vya maji sambamba na ukosefu wa Maji chini ya ardhi katika maeneo hayo.
Kwa sasa Mamlaka ya Maji ya Tunduma Kwa siku inazalisha mita za ujazo 823.83 wakati mahitaji katika mji wa Tunduma ni mita za ujazo 20,741.94 sawa na asilimia 44.5. Mamlaka pia inatoa huduma katika kata 10 kati ya kata 15 zenye idadi ya watu 226,434.
No comments:
Post a Comment