Kukamatwa kwa mshukiwa wa mauaji ya Kenya kumezua hisia kali kote nchini - baadhi ya watu wakihoji kuwa polisi wana maswali ya kujibu.
Polisi wanasema Collins Jumaisi Khalusha, 33, alikiri kuwaua wanawake 42 - lakini siku ya Jumanne wakili wake aliiambia mahakama kuwa aliteswa ili kukiri mauaji.
Ni taarifa ya hivi punde zaidi kuhusu tukio la kutatanisha lililofuatia ugunduzi wa mabaki ya miili tisa iliyokatwa vipande, kuwekwa kwenye mifuko, kufungwa kwa kamba na kutupwa kwenye machimbo ambayo hutumika kama jaa la taka karibu na kituo cha polisi mtaani Mukuru, jijini Nairobi.
Baadhi ya watu hawaelewi ni kwa vipi polisi hawakuweza kugundua kuwa miili ilikuwa ikitupwa karibu mita 100 kutoka kituo chao kilichopo katika mtaa wa mabanda wa Mukuru Kwa Njenga.
Wakazi wamewakosoa maafisa kwa "utepetevu" katika kushughulikia masuala ya uhalifu.
Kujibu hilo, Kaimu Mkuu wa Polisi Douglas Kanja siku ya Jumapili alitangaza kwamba maafisa wa kituo cha polisi cha Kware kilichopo karibu na eneo la tukio wamehamishwa.
Haijabainika ikiwa wamehojiwa jinsi mauaji hayo yalivyofanywa bila kutambuliwa.
Lakini kutokana na sifa mbaya ya kikosi cha polisi linapokuja suala la haki za binadamu, Mamlaka inayosimamia utendakazi wao ilisema inafanya uchunguzi kubaini ikiwa polisi walihusika kwa vyovyote na mauaji hayo.
Operesheni ya kuopoa miili kutoka kwenye chimbo hilo ilivutia mkusanyiko mkubwa wa watu
Kile kinachoshangaza zaidi ni jinsi wakazi walivyogundua mabaki hayo.
Familia ya Josephine Owino, ambaye alikuwa ametoweka, inasema alimjia "ndotoni" mmoja wao na kuwaelekeza kwenye jalala hilo.
Diana Keya, ndugu wa Bi Owino, aliiambia kituo cha Citizen TV kwamba familia iliwalipa vijana kupekua taka katika jalala hilo.
Hivyo ndivyo miili tisa iliyoharibika vibaya ilipatikana Ijumaa wiki iliyopita. Ilikuwa imefungwa kwenye mifuko ya plastiki kwa kutumia kamba.
Taarifa ya awali ya polisi ilisema "kisa hicho kiligunduliwa" na wakazi.
Alipoulizwa baadaye mkuu wa Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mohamed Amin alisema: "Sisi sio waotaji na hatuamini ndoto."
Polisi walisema miili iliyopatikana ilikuwa katika hatua tofauti za kuoza, na kuongeza kuwa waathiriwa walikuwa wameuawa nyakati tofauti.
Polisi pia wanasema mshukiwa Bw Khalusha alikiri kuwaua wanawake hao kwa kipindi cha miaka miwili, ushahidi ambalo sasa unatiliwa shaka.
Jambo ambalo haliko wazi ni iwapo mabaki hayo yalitupwa wakati huo au hivi karibuni.
Hussein Khalid, mkurugenzi mtendaji wa shirika la Haki Afrika, aliiambia BBC kwamba maelezo ya polisi kuhusu matukio hayo yalikuwa na "maswali mengi".
Jambo linalozua maswali ni jinsi polisi walivyofanikiwa kumkamata mshukiwa chini ya siku tatu baada ya kupatikana kwa miili hiyo ingawa hawakuwahi kutilia shaka tukio lolote lisilo la kawaida katika muda wa miaka miwili.
Jumatatu wiki hii, polisi walisema Bw Khalusha alikamatwa kwenye baa akitazama mechi ya fainali ya michuano ya Euro 2024.
Walionyesha kwenye vyombo vya habari baadhi ya vitu vinavyosemekana kupatikana kwa nyumba ya mshukiwa - pia karibu na mahali ambapo miili ilipatikana - ikiwa ni pamoja na simu 10, kipakatalishi, vitambulisho na nguo za ndani za kike.
Polisi walisema walifuatilia aliko Bw Khalusha baada ya kupata simu ya mmoja wa waathiriwa wake.
Wakili wa Bw Khalusha amehoji uhalali wa ushahidi huo.
Ni mwili mmoja tu uliotambuliwa kufikia sasa - wa Roseline Ongogo mwenye umri wa miaka 24.
Ndugu yake Emmanuel Ongogo ameiambia BBC kwamba alitoweka tarehe 28 Juni alipotoka nyumbani kwenda kutafuta kibarua.
Anasema familia yake ilienda chumba cha kuhifadhi maiti cha City ilipopata habari kuhusu miili iliyopatikana Mukuru.
Walimtambua kwa sababu alikuwa na nguo aliyokuwa amevalia na msongo wa nywele aliyokuwa nayo wakati alipotoweka.
Familia ya Roseline Ongogo ilikuwa ikimtafuta kwa zaidi ya wiki mbili
Polisi pia wanadai kuwa mke wa Bw Khalusha alikuwa mwathiriwa wake wa kwanza na wanasema kitambulisho chake kilipatikana miongoni mwa vitu vingine vinavyodaiwa kuwa vya waathiriwa.
Familia ya Bi Owino, iliyosema kuwa iliota kuhusu aliko, iliiambia BBC kuwa bado wanasubiri uchunguzi.
Kupatikana kwa miili hiyo kumeibua kumbukumbu ya mauaji ya kinyama ya mwezi Januari ya msichana Rita Waeni aliyekuwa na umri wa miaka 20.
Mwili wake uliokuwa umekatwa vipande ulipatikana katika nyumba ya kupanga kwa makazi ya muda mfupi jijini Nairobi. Kesi hiyo bado haijatatuliwa.
Kifo hicho kilisababisha maandamano nchini kote kupinga kuongezeka kwa visa vya mauaji ya wanawake na unyanyasaji dhidi yao.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilisema zaidi ya visa 500 vya mauaji ya wanawake vilirekodiwa nchini Kenya kati ya 2016 na 2023.
Miili yote iliyopatikana jalalani katika kisa cha hivi punde ni ya wanawake.
Viongozi wachache wa wanawake waliochaguliwa ambao walikusanyika katika chumba cha kuhifadhia maiti waliiomba serikali kuharakisha uchunguzi na kukomeshaukatili wa aina hiyo.
Alipoulizwa polisi walikuwa wakifanya nini kushughulikia kesi za mauaji ya wanawake na unyanyasaji dhidi ya wanawake, msemaji Resila Onyango alisema hawezi kushughulikia suala hilo haswa - lakini aliambia BBC kwamba kazi ya polisi ni "kulinda maisha na mali ya kila mtu".
No comments:
Post a Comment