MAHAKAMA YA KENYA YAAMURU MALIPO KWA MJANE WA MWANDISHI WA HABARI WA PAKISTANI ALIYEUAWA NA POLISI NCHINI HUMO. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, July 8, 2024

MAHAKAMA YA KENYA YAAMURU MALIPO KWA MJANE WA MWANDISHI WA HABARI WA PAKISTANI ALIYEUAWA NA POLISI NCHINI HUMO.

 


Mahakama nchini Kenya imetoa shilingi 10m ($78,000; £61,000) kama fidia kwa mjane wa mwanahabari maarufu wa Pakistani aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi kwenye kizuizi cha barabarani karibu miaka miwili iliyopita.


Arshad Sharif alikuwa mtangazaji wa televisheni anayejulikana kwa ukosoaji wake wa wazi dhidi ya viongozi wenye nguvu wa kijeshi wa Pakistani na ufisadi katika siasa.


Baba wa watoto watano alipokea vitisho vya kuuawa ambavyo aliviashiria kwa jaji mkuu wa Pakistan, kabla ya kutoroka nchi yake kutafuta usalama nje ya nchi. 


Mauaji ya Sharif miezi miwili baadaye mikononi mwa polisi katika mji wa Kajiado nchini Kenya yalisababisha ghadhabu, na jibu la polepole la maafisa lilifanya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuzikosoa Kenya na Pakistan.


Polisi wa Kenya walidai kuwa ni kisa cha utambulisho kimakosa lakini mjane wa Sharif, Javeria Siddique, alisema ni mauaji yaliyopangwa yaliyotekelezwa kwa niaba ya mtu ambaye hakutajwa jina nchini Pakistan.


Siku ya Jumatatu, Mahakama Kuu ya Kajiado iliamua kwamba mamlaka ya Kenya ilitenda kinyume cha sheria na kukiuka haki ya kuishi ya Sharif. Ilitoa uamuzi wa Bi. Siddique kupewa fidia pamoja na riba hadi malipo yakamilike.


"Hasara ya maisha haiwezi kufidiwa kwa njia za kifedha wala uchungu na mateso ambayo familia imepitia. Lakini kuna maafikiano kwamba fidia ni suluhu mwafaka kwa kukiuka haki za kimsingi," alisema Jaji Stella Mutuku alipokuwa akitoa uamuzi huo.


Jaji huyo pia aliamua kwamba mkurugenzi wa mashtaka ya umma nchini Kenya na mamlaka huru ya kusimamia polisi walikiuka haki za Sharif kwa kukosa kuwashtaki maafisa wawili wa polisi waliohusika. 


Mahakama imeamuru asasi zote mbili kukamilisha uchunguzi na kuwafungulia mashtaka maafisa hao.


Wakili anayemwakilisha mjane wa Sharif, Ochiel Dudley, alisema "huu ni ushindi kwa familia na ni ushindi kwa Wakenya katika harakati zao za kuwajibika kwa polisi".


Mjane wa Sharif, Bi Siddique, alitoa shukrani zake kwa mahakama ya Kenya lakini akaongeza kuwa kazi yake bado haijakamilika.

No comments:

Post a Comment